Na Mwandishi Wetu, Morogoro
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Tanzania Leaf Tobacco Company (TLTC) na Tanzania Tobacco Processors Limited (TTPL), Paul Crossan amewataka
wachezaji wa timu ya soka ya Tumbaku FC ya mjini hapa kuhakikisha wanajituma, ili kupata nafasi ya kushiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.
Crossan aliyasema hayo wakati akikabidhiwa kombe la mkoa wa Morogoro na timu ya Tumbaku, ambayo inamilikiwa na kiwanda hicho baada ya kumaliza wa kwanza katika ligi hiyo iliyomalizika hivi karibuni.
Mmeipa heshima kubwa kampuni na uongozi mzima kwa kushinda kikombe hiki na sisi tunawakikishia ushirikiano wa kila hali kuhakikisha mnashinda mashindano ya kanda na hatimaye kupata nafasi ya kushiriki Ligi Kuu, alisema.
Kwa upande wake Mkutugenzi wa TTPL, Dion Haigh aliwapongeza wachezaji hao kwa mafanikio waliyoyapata katika ligi hiyo, iliyohusisha timu sita na kusema kama si kujituma kwao basi wasingeweza kufikia hapo walipo.
Mmepiga hatua kubwa na sisi tutaendelea kushikirkiana na ninyi kuhakikisha kuwa mnafanya vizuri katika michuano ya kanda, lengo ni kuhakikisha kuwa mnapata nafasi ya kucheza Ligi Kuu katika siku za karibuni, alisema Haigh.
Alisema kampuni yake itaendelea kusaidia si tu timu ya soka bali na ile ya netiboli, lengo likiwa ni kuhakikisha wanakuwa na vikosi imara vitakavyoiletea sifa kampuni.
Naye Mkurugenzi wa Sheria na Uhusiano wa TLTC na TTPL, Richard Sinamtwa alisema ili kuhakikisha kuwa wanafanya mazoezi ya kutosha, uongozi wa kampuni hiyo umeanza ujenzi wa kituo cha michezo, ambacho kitagharimu sh. milioni 50 lengo likiwa ni kuwapatia wachezaji sehemu bora ya mazoezi.
Michuano hiyo ya mkoa ilianza hatua ya awali ikiwa na timu 86 ambazo zikipungua nakubaki sita zilizoshiriki katika fainali hizo ambazo ni Alliance One, Mkamba Rangers, Soko Stars, Mitumba, Dogs na Tumbaku FC.
No comments:
Post a Comment