LONDON, England
NAHODHA wa Chelsea, John Terry amesema kwamba bado ana matumaini ya kubeba kikombe cha Ligi ya England na michuano ya Klabu Bingwa Ulaya
msimu huu.
Kauli hiyo ya Terry, imekuja kutokana na mabingwa hao watetezi kurejea katika mbio za kutetea ubingwa wake baada ya kuwa katika kiwango chake kwa kushinda mechi tano mfululizo.
Kwa sasa Chelsea ambayo inashika nafasi ya nne ikiwa nyuma kwa pointi mbili dhidi ya Manchester City, ambayo inatarajiwa kukutana nayo, ipo nyuma kwa pointi nane dhidi ya vinara wa ligi hiyo Manchester United huku ikiwa na mechi moja mkononi.
Lakini Terry alisema juzi kuwa hawataki kusamehe mbio hizo wala kuacha mapamabano. "Sote tunaweza kushinda mechi zetu, tutaendelea kupigana hadi mwisho ili tuweze kuona kitakachotokea," alisema Terry.
"Mashabiki wetu bado wameweka matumaini yao kwetu msimu huu, tumeshawaahidi mashabiki kumaliza msimu huu tukiwa na nguvu na kiwango tulichoonesha tunaweza kupata matokeo mazuri," aliongeza.
Mbali na Ligi Kuu, beki huyo wa timu ya taifa ya England vilevile alisema wanataka kupeleka taji la michuano ya Klabu Bingwa Ulaya Stamford Bridge.
Blues hivi sasa ipo katika nafasi nzuri ya kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo, wakati itakapoikaribisha Copenhagen ya Denmark katika mechi ya marudiano ya hatua ya 16 bora na kutokana na mazingira hayo, Terry alisema bado msimu huu ni mziri kwao na wapo tayari kwa mapambano.
No comments:
Post a Comment