Na Zahoro Mlanzi
KATIKA kile kinachoonekana timu ya Simba, kuvutiwa na mazingira ya jijini Arusha, wekundu hao wa Msimbazi sasa wameamua kupumzika kwa
muda jijini humo.
Simba ilikwenda Arusha kuumana na Arusha FC, katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara, kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Cliffold Ndimbo, alisema timu hiyo jana ilikuwa na mapumziko, lakini leo wanaendelea kujifua kama kawaida kujiandaa na mchezo wao dhidi ya mabingwa watetezi wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika, TP Mazembe.
"Tunatarajia kurudi jijini Dar es Salaam katikati ya wiki, nimezungumza na kocha Phiri (Patrick), akaniambia bado wapo Arusha wanapumzika, ila siku si nyingi watarudi kuendelea na taratibu nzima ya safari," alisema Ndimbo.
Akizungumzia tetesi za timu yao kuweka kambi tena visiwani Zanzibar, alisema kutokana na muda ulivyokwenda, hana uhakika kama timu hiyo itakwenda visiwani huko.
"Kama nilivyosema tunarudi Dar es Salaam katikati ya wiki, sidhani kwa siku zitakazobaki kama tutakuwa na muda wa kwenda Zanzibar, siku zitakazobaki zitatumika kwa ajili ya maandalizi ya safari," alisema Ndimbo.
Kwa ushindi walioupata Simba dhidi ya Arusha FC, sasa imebakiza pointi sita kufikisha pointi 60, ambazo hazitafikiwa na timu yoyote, hivyo itakuwa imetwaa ubingwa kwa mara ya pili mfululizo.
Yanga ambayo ipo katika nafasi ya pili, inaiombea mabaya Simba ipoteze michezo miwili ili nayo ikishinda michezo yao mitatu, ifikishe pointi 49, ambapo Simba haitakuwa na uwezo wa kuzifikia.
No comments:
Post a Comment