07 March 2011

Serikali kuanzisha mfumo wa taarifa za ajira

Na Grace Michael

WIZARA ya Kazi na Ajira inatarajia kuanzisha mfumo bora wa utoaji wa taarifa za soko la ajira ambao utasaidia watu binafsi, taasisi za elimu na mafunzo kutoa
taaluma zinazohitajika kwa sasa na baadaye katika soko la ajira.

Uanzishwaji wa mfumo huo unatokana na sera ya ajira iliyopo kutokidhi baadhi ya mahitaji ya mabadiliko ya ukuaji wa haraka wa nguvu kazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia hasa teknolojia ya habari ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza idadi ya ajira.

Akizungumzia uanzishwaji wa mfumo huo, Waziri wa Kazi na Ajira Bi. Gaudensia Kabaka Dar es Salaam jana, alisema kuwa soko la ajira ni mfumo wa mahusiano kati ya mahitaji ya ajira na fursa za ajira zilizopo lakini pia ndicho kigezo kikubwa kinachotoa picha halisi ya mafanikio ya kiuchumi na kimaendeleo.

Katika taarifa za soko la ajira tunatarajia kuona takwimu zinazohusu hali ya nguvu kazi kwa maana ya kiwango cha upatikanaji wa ajira, ukosefu wa ajira, ajira isiyo timilifu, ujira kwa kazi, mchanganuo wa mapato na umasikini, hali ya elimu nchini, muda wa wastani kwa wahitimu kupata ajira kulingana na fani au ujuzi unaohitajika katika soko la ndani na nje ya nchi, alisema Bi. Kabaka.

Mbali na hayo pia mfumo huo utawezesha kujua hali ya ajira kwa wageni kutoka nje ya nchi na fani au ujuzi ambao haupatikani hapa nchini, pia nafasi za ajira zilizopo nje ya nchi na fani au ujuzi unaohitajika.

Bi. Kabaka alisema kuwa taarifa hizi zitaisaidia serikali katika maamuzi mbalimbali yakiwemo ya kuridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa kama ya Soko la Pamoja la Afrika Mashariki, kufungua mipaka kuhusu masuala ya ajira kwa fani na ujuzi unaokosekana nchini na aina ya kazi na fani ambazo Tanzania inaweza ikanufaika katika ushirikiano huo.

Vyanzo vya sasa vya taarifa za soko la ajira vimeshindwa kuwa na viwango vinavyotakiwa vya utoaji wa taarifa sahihi za mara kwa mara na hivyo kutokidhi mahitaji ya kusaidia utoaji wa maamuzi yanayohusu sera na mikakati mbalimbali ya maendeleo, alisema Bi. Kabaka.

Alisema kuwa kwa kuliona hilo, Wizara ya Kazi na Ajira kwa kushirikiana na Shirika Kazi Duniani (ILO), Vyama vya waajiri na waajiriwa imeamua kushughulikia suala hilo la upatikanaji wa taarifa sahihi za soko la ajira kwa kuweka mfumo wa kitaifa wenye ufanisi, na wa gharama nafuu utakaowezesha upatikanaji wa taarifa sahihi na kwa wakati.

Alisema kuwa mchakato umeanza kwa kufanya majadiliano na wadau na mambo yaliyokubalika ni kuandaa mwongozo wa kitaifa kuhusu ukusanyaji, uchambuzi na utoaji taarifa za soko la ajira na mfumo huo unatarajiwa kuanza kutumika Juni mwaka huu.

No comments:

Post a Comment