Na Heckton Chuwa, Moshi
MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, (KKKT), Dkt. Alex Malasusa ameelezea kusikitishwa kwake na umasikini unaozikumba nchi nyingi ambao alisema
husababishwa na matumizi makubwa ya fedha kwa ajili ya tiba za wananchi.
Askofu Dkt. Malasusa alitoa kauli hiyo wakati akitoa salamu kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 40 tangu kuanzishwa kwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC jana ambapo alipendekeza nguvu kubwa ziwekwe katika kufanya utafiti.
Fedha nyingi za maendeleo zinapelekwa kwenye tiba hivyo kusababisha umasikini kwa nchi nyingi masikini, hapa kinachohitajika ni mamlaka husika kujikita katika kufanya tafiti mbalimbali ili kubaini vyanzo vya maradhi na hatimaye kuviangamiza, hii itasaidia zaidi, alisema.
Dkt. Malasusa alisema kuwa amekuwa akishiriki mara nyingi katika kugawa vyandarua kwa ajili ya kuzuia malaria na kuona gharama kubwa zinavyotumika na kushauri ya kuwa pamoja na kuwa kazi hiyo inalenga kuzuia ugonjwa huo, gharama kama hizo pia zingetumika katika kufanya utafiti na kuangamiza mazalia ya mbu.
Wakati huo huo, Dkt. Malasusa aliipongeza serikali ya Rais Jakaya Kikwete kwa ushirikiano wake inaoutoa kwa taasisi za kidini katika kutoa na kuboresha huduma za afya nchini.
Dkt. Malasusa alitoa pongezi hizo wakati akizindua Harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa wodi mpya katika hospitali hiyo.
Pamoja na ufinyu wa bajeti yake, serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kuboresha afya za wananchi wake bila kujali itikadi zao, hili ni jambo la kupongezwa kwa dhati, alisema na kuongeza kuwa fedha hizo ni pamoja na mishahara ya wafanyakazi pamoja na za kunulia dawa na vifaa vya tiba.
Dkt. Malasusa ambae pia ni mwenyekiti wa shirika la Msamaria Mwema, (GSF), ambao ni wamiliki wa Hospitali ya KCMC, aliendelea kusema kuwa changamoto zinazoikabili hospitali hiyo ni za kila mmoja kutokana na umuhimu wa taasisi hiyo katika kutoa huduma zake ambazo kwa sasa zimewalenga hata wagonjwa kutoka nje ya nchi.
Kila mmoja ana uwezo wa kuchangia kuboresha huduma hapa KCMC hivyo basi hatuna budi kuepuka dhana kuwa kazi hiyo inawezwa kufanywa na mtu mmoja au taasisi moja, kila
mtu achange kadiri ya uwezo wake, alisema.
Awali mkurugenzi mtendaji wa hospitali ya KCMC Dkt. Moshi Ntabaye, alisema changamoto kubwa inayoikabili hospitali hiyo ni ufinyu wa vitanda pamoja na vifaa vya tiba, ambavyo alisema vingi vimechakaa.
Dkt. Ntabaye ambae pia ni katibu mkuu wa GSF, alisema kuwa zinahitajika sh. bilioni 15 ili kufanikisha ukarabati na ujenzi wa majengo mapya hospitalini hapo.
No comments:
Post a Comment