*SBL 'yaitia ndimu' taifa Stars
Na Zahoro Mlanzi
KOCHA Mkuu wa timu ya taifa 'Taifa Stars', Jan Poulsen amesema ni lazima waifunge Jamhuri ya Afrika ya Kati ili wawe katika nafasi nzuri ya kuwania
kuzufu fainali za Mataifa ya Afrika.
Mbali na tambo hizo, Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), imetoa sh. milioni 100 kwa timu hiyo katika maandalizi ya mchezo huo ikiwa ni moja ya utekelezaji katika mkataba wao na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Timu hizo zinatarajiwa kuumana kesho kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo Afrika ya Kati ndiyo kinara wa Kundi lao la D na Taifa Stars ipo nafasi ya tatu.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Poulsen alisema kuwemo katika mbio za kufuzu ni lazima waifunge Afrika ya Kati na hiyo ni kutokana na nafasi waliyopo katika kundi lao.
"Jamhuri ya Afrika ya Kati ni timu nzuri na sijawahi kuiona kabla, ila kwa michezo waliyocheza ndiyo nimeweza kuijua, tutatumia nafasi ya kuwa nyumbani kuibuka na ushindi," alisema Poulsen.
Alisema wachezaji wake wamejiandaa vizuri katika mchezo huo na kwamba kikubwa Watanzania wajitokeze kwa wingi kuishangilia timu yao kwani wachezaji wameahidi kujituma kwa nguvu zao zote.
Naye Nahodha wa timu hiyo, Shadrack Nsajigwa amewaomba Watanzania wawaombee katika mchezo huo waibuke na ushindi, kwani wakishinda watakuwa katika nafasi nzuri ya kufuzu michuano hiyo.
Wakati huo huo, Kocha Mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jules Accorsi ametamba kwamba timu yake ina uwezo wa kufuzu kwa fainali hizo kutokana na uwezo wa vijana wake.
Alisema amekuja nchi kuhakikisha timu yake inashinda na anajua mchezo unaweza kuwa na matokeo mengine mawili ya kufungwa au sare, hivyo matokeo yoyote yanaweza kutokea.
Katika hatua nyingine, Meneja wa Bia ya Serengeti, Allan Chonjo amekabidhi mfano wa hundi ya sh. milioni 100 kwa TFF kwa ajili ya maandalizi ya timu ya taifa katika mchezo huo.
Alisema wapo pamoja na Watanzania wote na anawaomba wajitokeze kwa wingi kuipa sapoti Taifa Stars, kwani jitihada zao zinaweza kuzaa matunda na hatimaye kuibuka na ushindi.
chezeni mpira acheni na habari za watanzania mtuombee. kila kitu mnataka Mungu ndiye afanye. acheni hizo. maana kila siku kuomba Mungu tuu bila ya jitihada, Mungu hamsaidii mvivu.
ReplyDelete