Na Mwandishi Wetu
JESHI la Polisi nchini linatarajia kuteketeza mabomu katika maghala ya Zanzibar yaliyokaguliwa na kubainika muda wake umeshakwisha.Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana
na Mtaalamu wa mabomu ACP Lufenta Mwamzi kwenye warsha ya uhamasishaji vyombo vya habari juu ya kukabiliana na tatizo la uzagaaji wa silaha ndogondogo na nyepesi.
"Jopo la wataalamu wa mabomu kutoka taasisi za ulinzi na usalama tumekwenda Zanzibar na tumegundua kuwa kuna mabomu mengi kwenye maghala ambayo muda wake umepita na hivyo kutakiwa kuyateketeza," alisema ACP Mwamzi.
ACP Mwamzi alisema zoezi hilo kwa Zanzibar litaanza rasmi Aprili 8, mwaka huu na hivyo kuwataka wananchi wasipatwe na mshtuko kutokana na zoezi hilo.
Aliongeza kuwa zoezi hilo litaenda sambamba na ukaguzi wa silaha zisizolipiwa ada, ambapo imebainika kuwa ni asilimia 25 tu ya wamiliki wenye silaha ambao wamelipa ada zao.
"Zoezi la uteketezaji mabomu utaenda sambamba na wasiolipa ada za silaha zao na zoezi hili linatarajia kuanza Aprili Mosi mwaka huu na litakuwa ni Mkoa kwa Mkoa," alisema.
Awali akifungua warsha hiyo Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini Robert Manumba alitumia wakati huo kuwatumia salamu wahalifu na kusema Jeshi la Polisi halina mzaha wala utani na wahalifu na hivyo kuwataka watafute kazi nyingine.
Manumba alisema uzagaaji wa silaha ndogondogo nchini na Ukanda wa Maziwa Makuu ni chanzo cha uhalifu wa kutumia silaha na hivyo ni muhimu kwa wananchi kuwa wazelendo.
Aidha alisema ni muhimu kuelewa uhalifu wa kimataifa kwa matumizi mabaya ya silaha, kwani yanatumika zaidi Afrika wakati yenyewe haitengenezi silaha.
Aliwataka wananchi wa mipakani kuwakataa na kuwakumbatia wahalifu kwa kutegemea kamisheni ya wahalifu, kwani watambue risasi haitambui mtu.
"Nawaomba wananchi wa mipakani kuacha tabia ya kuwakumbatia wahalifu, kwani silaha nyingi hupitia katika maeneo yao, na watambue kuwa wahalifu ni hatari kwa maisha ya walio wengi," alisema Manumba.
Hata hivyo, tayari jeshi hilo limeanza kuzitambua na kuzipa alama maalumu silaha zote zinazomilikiwa na taasisi za serikali na watu binafsi, ambapo kwa sasa tayari wameshaanza katika Mikoa ya Kipolisi ya Jiji la Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment