11 March 2011

Nchi wanachama EAC kitanzini

*Zalia na hukumu ya fidia bilioni 180/-

Na John Daniel

NCHI wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki huenda zikalazimika kulipa fidia ya zaidi ya sh. bilioni 180 kupitia Benki ya Afrika Mashariki (EADB) kwa
kampuni ya Blueline Enterprises Limited ya Tanzania.

Malipo hayo yanatokana na uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania katika kesi iliyofunguliwa na EADB baada ya kampuni hiyo kushindwa kulipa mkopo wa zaidi ya dola milioni 2.2.

Kutokana na uamuzi huo baadhi ya nchi wanachama wa Jumuiya hiyo wameinyoshea kidole Tanzania kuwa haijasimamia kikamilifu mkondo wa sheria kulinda benki hiyo huku baadhi wakitaka tawi la benki hiyo Tanzania lifungwe iwapo serikali itakaa kimya hadi EADB ikalipa fedha hizo.

Benki hiyo huendeshwa kwa kuongezewa mtaji na nchi wanachama kila mwaka kutokana na kodi za wananchi husika.

Katika mwaka wa Fedha 2010/2011 Tanzania ilichangia dola milioni 6.3 (zaidi ya sh bilioni 9) kuongezea mtaji.

Kwa mujibu wa nyaraka zilizopatikana kutoka Mahakama ya Rufaa nchini, EADB iliamuriwa kuilipa kampuni hiyo dola za Marekani milioni 129 zaidi ya sh. bilioni 180 za Tanzania baada ya kushinda kesi, hali ambayo inaiweka pabaya benki hiyo kwa upande wa Tanzania.

Kwa mujibu wa nyaraka hizo za Mahakama ya Rufaa, EADB iliingia mkataba wa kuikopesha Blueline Enterprises Limited dola za Marekani milioni 2.2 Machi 7, 1990 kwa makubaliano ya kulipa kwa muda wa miezi 36.

Kampuni hiyo ililipa sehemu ya mkopo wake lakini haikumaliza kwa mujibu wa makubaliano, jambo liliilazimu benki hiyo kufungua kesi kudai haki yake lakini ikageuziwa kibao na kujikuta katika wakati mgumu.

Kwa mujibu wa hukumu hiyo, Mahakama Kuu ya Tanzania inalalamikiwa kuwa hukumu yake haikuitendea haki EADB kwa kuipa ushindi kampuni hiyo ambayo ilikuwa ikidaiwa na benki hiyo.

Katika hukumu hiyo iliyotolewa Novemba 15, 2006, Jaji Augustine Shangwa wa Mahakama Kuu ya Tanzania aliamuru kampuni hiyo kukamata dola za Marekani 68,546,653.00 za EADB zilizokuwao katika Benki ya Standard Chartered jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, EADB ilishtukia hukumu hiyo na kufungua kesi nyingine kupinga uamuzi huo chini ya sheria iliyoanzisha benki hiyo, inayotoa kinga kwa mali za benki hiyo kukamatwa.

Uamuzi wa Jaji Shangwa dhidi ya EADB ulipingwa na washirika wa maendeleo wa kimataifa ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB), Benki ya PTA na nchi zinazochangia bajeti ya serikali.

Tayari EADB imeomba Mahakama ya Rufaa Tanzania kufanya mapitio katika vifungu kadhaa vya mwenendo wa kesi hiyo kwa kuwa haikuridhika na maamuzi yaliyotolewa na kwamba wakati wa kesi hiyo haikupewa haki ya kusikilizwa kikamilifu.

Taarifa kutoka ndani ya EADB tawi la Tanzania na Makao Makuu nchini Uganda zilieleza kuwa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania imepokea na kukubali kuanza kusikiliza mapitio ya rufaa ya beki hiyo Aprili 6, mwaka huu.

Waanzilishi wa EADB ni serikali za Tanzania, Kenya na Uganda. Pia zipo nchi wahisani wenye hisa katika benki hiyo waliosaidia kuanzishwa kwake ikiweko Japan. Kwa sasa nchi ya Rwanda pia ni mwanachama katika benki hiyo baada ya kujiunga rasmi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Akizungumza na Majira jana, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa EADB, Bw. Ramadhan Kijjah, alikiri kwamba uamuzi huo wa mahakama umeleta mkanganyiko na kwamba benki hiyo inasubiri mapitio ya rufaa.

"Ni kweli kesi hiyo iliamuriwa hivyo na imeleta msuguano wa kisheria, sheria iliyoanzisha benki hiyo tangu miaka ya sabini inazuia mali zake zikiwemo fedha kukamatwa, lakini wanasheria walidai fedha zinaweza kukamatwa.

"Ni kweli suala hili halijakaa vizuri hata kwetu kama nchi lakini ni la kisheria tusubiri tu tutapata jibu la mwisho, "alisema Bw. Kijjah na kuongeza.

"Benki hiyo inatusaidia katika miradi mingi ya maendeleo, kila mwaka nchi inachangia na mwaka 2010/2011 Tanzania imechangia dola milioni 6,325,769, mchango wa mwaka huu bado ndio bodi inakutana kule Kigali kutoa bajeti," alisema.

Hata hivyo alisisitiza kuwa iwapo fedha hizo zitalipwa, nchi zote zitawajibika kwa kuwa EADB si mali ya Tanzania peke yake, bali ni nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kwa upande wake Waziri wa Fedha na Uchumi, Bw. Mustafa Mkulo, alisema hakuna fedha za walipa kodi ya Tanzania itakayotumika kulipa fidia hiyo kwa kuwa ni mali ya Jumuiya na si Tanzania kama taifa moja.

"Hakuna njia ambayo serikali ya Tanzania pekee italipa fedha hizo, ni lazima benki ibebe mzigo wake kutokana na makosa yake," alisema Bw. Mkulo.

Akizungumza na Majira kwa njia ya simu kutoka Mwanza, Waziri wa Ushiruikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Samuel Sitta, alikiri kwamba uamuzi huo wa Mahakama Kuu ya Tanzania umeleta mshtuko mkubwa katika vikao vya jumuiya hiyo kuhusu EADB lakini ni suala la kisheria.

"Kwa nchi inayoheshimu utawala wa sheria kama Tanzania  serikali haiwezi kuingilia suala hilo, ni lazima isubiri tu mpaka hatua ya mwisho, ni kweli suala hilo linaumiza sana lakini tunasubiri tu uamuzi wa mwisho wa mahakama," alisema Bw. Sitta.

Alisema suala hilo lilianza kujadiliwa katika vikao vya Jumuiya hiyo hata kabla yeye hajapewa wizara hiyo na kwamba hakuna njia ya kuingilia zaidi ya kuheshimu mhimili hiyo ya dola kutimiza wajibu wake kisheria.

Alikiri kwamba zipo nchi wanachama zinazoilalamikia serikali ya Tanzania kuhusu suala hilo lakini akasisitiza kuwa nchi huendeshwa kwa kuheshimu utawala wa sheria na kamwe haiwezi kuyumbishwa katika suala hilo la kusimamia haki na kuheshimu mahakama.

Mkurugenzi Mkuu wa EADB, Bi. Vivian Apopo hakupatikana kuzungumzia suala hilo baada ya Majira kujibiwa kuwa hayupo ofisini kwake Jijini Kampala kuhudhuria Kikao cha Bodi ya Bajeti ya Benki hiyo nchini Rwanda ambako simu yake ya mkonomni haikuwa hewani.

No comments:

Post a Comment