11 March 2011

Maduka yanayouza sukari zaidi ya 1,700/- kufungiwa

Na Tumaini Makene

WIKI mbili tangu serikali itoe bei elekezi ya sukari ya sh. 1,700, sasa imetoa agizo kwa watendaji wake wa ngazi ya wilaya, kusimamia kikamilifu suala hilo, la sivyo
wataadhibiwa wao.

Agizo hilo la Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Dkt. Cyril Chami limekuja siku kadhaa mara baada ya baadhi ya vyombo vya habari, likiwemo Majira, kuweka wazi namna wasambazaji wakubwa wa sukari wanavyohodhi sukari, ili ionekane kuna upungufu na wao wanufaike kwa bei ya juu.

Akizungumza na Majira jana, Dkt. Chami alisema kuwa maafisa biashara wa mikoa yote nchini wanatakiwa kushirikiana na ofisi za wakuu wa mikoa kukamata leseni ya mfanyabiashara yeyote wa rejareja anayeuza kilo ya sukari kwa zaidi ya sh. 1,700.

Aliongeza kuwa Ofisa Biashara wa Mkoa atakayeshindwa kutimiza agizo hilo atabadilishwa kazi, kisha eneo husika kupelekwa mtu mwingine anayaweza kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Juzi Majira liliripoti kuwa ukosefu wa sukari unaoonekana  nchini na kusababisha bei kupanda hauna ukweli kwani unasababishwa na 'janja' ya wasambazaji wakubwa wa sukari nchini, wanaotaka kujinufaisha kupitia migongo ya Watanzania maskini.

Vyanzo vya habari vya kuaminika vya Majira, vilisema kuwa baadhi ya wasambazaji wa sukari nchini ndiyo wanaohusika katika kuendelea kuhodhi bidhaa hiyo na kuifanya adimu, ili wao waendelee kunufaika kibiashara.

Imeelezwa kuwa uhaba huo wa sukari sasa unaonekana kuwa ni wa kutengenezwa kwa manufaa ya kikundi cha wafanyabishara wachache wakubwa wanaotaka kujinufaisha kwa gharama ya Watanzania.

Mpaka sasa wazalishaji wakubwa wa sukari nchini ni viwanda vya TPC (Moshi), Mtibwa, Kilombero na Kagera. Wasambazaji wakubwa ni Mohamed Enterprises Limited (METL), Al Neem, TPC Distributors na Lake Zone.

Mwishoni mwa Februari, serikali, kwa kuzingatia masuala yote ya kibiashara, kuanzia kwa mzalishaji, msambazaji hadi muuzaji wa mwisho, ilielekeza kuwa bei ya sukari haipaswi kuuzwa zaidi ya sh. 1,700, kwa bei ya rejareja kwa mtumiaji popote alipo nchini.

Akitangaza uamuzi huo ambao ulitokana na kikao kati ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda na wadau wote wa sukari nchini, Dkt. Chami alisema kuwa;

Katika tamko hilo, serikali ilifuta ushuru wa forodha kwa kiasi cha tani 37,500 kati ya tani 50,000 zitakazoagizwa kutoka nje ya nchi, ili kufidhishia hitaji la tani 50,000, kufidishia pengo la mahitaji kwa Mei hadi Juni, wakati uzalishaji wa viwanda vya ndani utakapoanza tena.

Moja ya sababu inayodhihirisha kuwa wasambazaji ndiyo wanaendeleza tatizo la sukari nchini kwa sasa, ni kushuka kwa mauzo kwa tani kwa baadhi ya wazalishaji tangu kutolewa kwa tamko hilo.

Taarifa zimeeleza kuwa mmoja wa wazalishaji wakubwa wa sukari hapa nchini, kabla ya tamko, alikuwa akiuza takribani tani 300 kwa siku, lakini baada ya serikali kuondoa ushuru wa forodha ili sukari iagizwe kwa wingi zaidi kuondoa upungufu mkubwa, mauzo hayo yameshuka zaidi ya nusu, mpaka kufikia tani 125.

"Maana yake ni kwamba sasa hawanunui tena sukari kutoka kwa wazalishaji (viwandani), sasa wanauza sukari waliyokuwa wamehodhi kabla, ili itakapoanza kuingia ile ya kutoka nje iliyoondolewa ushuru, waliyokuwa nayo isije ikawadodea, kilisema chanzo chetu cha habari.

Katika hatua nyingine, John Gagarini anaripoti kutoka Kibaha kuwa Mkuu wa mkoa wa Pwani, Bi Amina Said ameagiza sukari mkoani humo kuuzwa sh. 1,700 la sivyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Kibaha kwenye mkutano na waandishi wa habari na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Pwani, Bi. Saidi alisema kuwa hakuna sababu yoyote inayowafanya wafanyabiashara hao kuuza zaidi ya bei hiyo.

"Tayari tumeshakaa na wakuu wa wilaya zote za mkoa huu kwa ajili ya kutoa maelekezo kwa wafanyabiashara wa maeneo yao  kwa ajili ya bei halali iliyowekwa, hivyo tunaomba wafanyabiashara wafuate utaratibu uliowekwa na serikali," alisema Bi. Said.

7 comments:

  1. Mnalinda viwanda vya ndani au mnalinda wezi? mmepandisha ushuru wa sukari kwa makusudi ili kuvilinda viwanda vya washenzi hawa wenye tamaa ya utajiri,punguzeni ushuru na acheni wenye uwezo wa kuagiza sukari nje wafanye hivyo kama hatukununua sukari chini ya shilingi alfu moja,ulaya wanalinda viwanda vyao visife kwa sababu viwanda vinakidhi mahitaji yao,wewe leo unalinda kiwanda ambacho hakizalishi cha kutosha kwa wananchi.TOKA MWANZO TUMESEMA HAYO HAKUNA SHORTAGE YA SUKARI NA ILIYOKO NI YA KUTENGENEZWA ILI BEI IPANDE NA IKISHAPANDA HAISHUKI,SERIKALI IKO USINGIZINI HAMFANYI UKAGUZI WA GHAFLA KWENYE MAGHALA KWA SABABU LABDA MNA MASLAHI BINAFSI HUKO KWA WAFANYABIASHARA YA SUKARI

    ReplyDelete
  2. wa hili serikali inajaribu kuwahadaa wananchi. Wafanyabiashara ni watanzania na wazalendo kama watu wengine. Iwapo gharama za umeme, mafuta, nauli, vyakula na huduma nyingine zimepanda kiasi cha kutisha, je Dk. anataka wafanyabiashara waishi je? Kwa waziri wa wizara kama yako na msomi kama wewe unapaswa kuelewa iwapo sukuri ni haba maagizo yako yote yatagonga ukuta. CCM imevuruga uchumi ili kushinda uchaguzi wa 2010 haya sasa ni matokea ya fedha nyingi zilizoingizwa kwenye mzunguko kwa kununu kura bila uchumi kukua na hiyvo mfumuko wa bei uko juu. Iwapo CCM na Chami mtaendelea kung'ngania kushusha bei ya sukari kimabavu, basi hata hiyo iliyoko itaingia kwenye soko la magendo. Chami nadhani unafahamu wazi kwamba suluhisho tu ni kupunguza mfumuko wa bei na kuongeza upatikanaji wa sukari, vinginevyo ni ulaghai kwa wananchi. Kwa hili CCM inakimbia kivuli chake cha ubadhirifu na ufisadi.

    ReplyDelete
  3. Ndugu naomba tuwe wakweli kwenye hili ni leo tu bei ya sukari kwenye international market ni $809.75/ton (sawa na Tshs. 1'215'000/= ambayo ni Tshs 1'250/= kwa kilo) Brown Sugar huko Brazil. sasa naomba kujua bei ya tani moja itakuwaje hata baada ya kuwave out TAX.

    ReplyDelete
  4. Ndugu hapo juu... weka usafiri, clearing charges, storage, packing in small quantities, taxes nazo ni mlolongo, umeme, gharama za leseni na juu yake, mfumuko wa bei, kuanguka kwa shiling, faida vyote hivyo vinatosha kuifanya kilo moja kuwa 2200/=

    ReplyDelete
  5. Ni kwa nini Watz mkijadili matatizo lazima muweke habari ya uchaguzi? uchaguzi umeisha pita na aliyepata kapata na liyekosa kakosa,its over tujadili matatizo yetu. Ndugu hapo juu kwa nini utoe bei ya mbali kote huko usitoe ya hapo kenya au Zambia ambapo Customs kila siku wanakamata sukari zinazopitishwa kwa magendo,kama ingekuwa ni ghali huko ni kwa nini wafanyabiashara wanaenda kununua huko?
    ni lazima pana faida wakiuza. Sukari Tz iko juu sana ukichangia na mfumo mbovu wa uchumi ndio kabisa wananchi wanaangamia

    ReplyDelete
  6. Uchaguzi umetusababishia adha kubwa. wewe unafikiria uchaguzi ni ile siku unayotumbikiza kile kipande cha karatasi kwenye debe? Nadhani hapo umepotoka, uchaguzi umevuruga uchumi kwa matumizi ya kifisadi ambayo sasa bei kama sukari zanapaa kwa mfumuko mkubwa uliosababishwa na kutafuta ushindi kwa fedha! Sasa kama unajua jirani zetu bei zao ni chini, je hicho unachokiita mfumo mbovu nini? Sio hao mafisadi wa CCM?

    ReplyDelete
  7. Wenye viwanda vya Sukari wamechangia CCM kwenye hela za Uchaguzi. Hivyo wenye viwanda wanarudisha hela zao. nao CCM wakagawa kanga, kofia na pombe kwa wapiga kura wapumbavu. Wajinga ndo waliwao, acha tuumie sote halafu next time tutie akili.

    Pia tuache woga, CCM waliiba kura/kuchakachua, badala ya kuingia barabarani kupinga huu ujinga, eti tunadanganywa na amani. Amani iko wapi wakati kila uchao maisha yanazidi kuwa magumu??

    Heri kuandamana kuwang'oa hawa mafisadi kuliko amani isiyo na haki, amani ya mateso kwa walalahoi.

    ReplyDelete