02 March 2011

Mkutano Mkuu Yanga waota mbawa

*Waelekeza nguvu mechi ya Simba

Na Elizabeth Mayemba

MKUTANO Mkuu wa dharura wa Yanga ambao wanachama waliuomba umeota mbawa, baada ya Kamati ya Utendaji iliyokutana
Jumamosi kushindwa kuuzungumzia.

Awali Mwenyekiti wa klabu hiyo, Lloyd Nchunga alikaririwa katika vyombo vya habari kwamba mkutano huo, ungefanyika mara baada ya mchezo wao dhidi ya Kagera Sugar.

Habari zilizopatikana Dar es Salaam jana kutoka kwa baadhi ya wajumbe waliohudhuria kikao hicho wameeleza kuwa katika kikao hicho hakukuwa na ajenda yoyote inayohusu mkutano huo.

"Katika kikao chetu tulizungumza mambo mbalimbali, lakini hatukuthubutu kuzungumzia suala lolote la Mkutano Mkuu, kwani muda wa kufanya hivyo bado," alidai mmoja wa wajumbe hao ambaye hakutaka jina lake.

Alisema kamati hiyo inautambua Mkutano Mkuu wa kikatiba ambao hufanyika kila mwaka na mkutano huo bado haujapangiwa tarehe kwa kuwa sasa hivi timu inakabiliwa na mechi mbalimbali za Ligi Kuu ya Vodacom.

Mjumbe huyo alidai kwamba suala la Mkutano Mkuu ni la kikatiba zaidi na kama wajumbe wanalitambua hilo, hivyo muda utakapofika utafanyika kwa mujibu wa kanuni.

Awali baadhi ya wanachama wa klabu hiyo waliibuka na kuutaka uongozi wa klabu hiyo kuitisha Mkutano Mkuu wa wanachama haraka ili kuondoa malumbano ya viongozi ambao walikuwa hawaelewani na pia suala Mjumbe wa Bodi ya Udhamini ya Yanga, Yusuf Manji ambaye amekabidhi barua ya kujiudhulu.

Mjumbe huo pia walidai kuwa katika kikao hicho walipanga mikakati ya timu ili iweze kushinda mechi zote zilizosalia za Ligi Kuu ya Bara.

"Mechi zinazofuata ni ngumu, hasa kwa Simba na Azam FC, hivyo nguvu zote zimeelekezwa kwenye mechi hizo kwani kama tukipoteza michezo hiyo ndoto zetu za kutwaa ubingwa zitaota mbawa," alisema mjumbe huyo.

Alisema kwa sasa wanatumia muda mwingi kufikiria mechi zilizosalia kwa kuwa mzunguko huu ni wa lala salama na kila timu inataka kutwaa ubingwa.

Wakati huo huo, Yanga iliondoka jana Dar es Salaam kwenda mjini Bagamoyo kwa ajili ya kuweka kambi ya kujiandaa na mchezo wao dhidi ya Simba, unaotarajiwa kuchezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment