Na Suleimani Abeid, Shinyanga
MBUNGE wa Jimbo la Kawe, Bi. Halima Mdee aliwataka wananchi kukinga mkono Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kupuuza
kauli zinazotolewa na viongozi wa CCM na wale wa serikali yake kuhusu kufanyika kwa maandamano na mikutano ya chama hicho .
Akizungumza katika mkutano uliofanyika jana mjini Mwanhuzi wilayani Meatu mara baada ya maandamano makubwa yaliyofanyika katika mji huo, Bi. Mdee alisema maneno mengi yanayotolewa na vigogo wa CCM kama husani hotuba ya Rais Jakaya Kikwete yamelenga kutaka kuwatia hofu isiyo na sababu Watanzania ili vigogo hao waendelee kufaidi matunda ya nchi hii peke yao.
Alisema hivi sasa Watanzania wanakabiliwa na matatizo chungu nzima ikiwemo ukosefu wa nishati ya umeme lakini serikali ya CCM imeshindwa kuwatatulia matatizo hayo, lakini CHADEMA tunaieleza serikali ya Kikwete kuwa kizazi hiki cha leo siyo kile cha jana, ni kizazi cha ‘digital’ na siyo cha ‘analogy’ kilichopitwa na wakati.
“Tunawaeleza CCM na Kikwete kama hawataki kuona maandamano na mikutano hii ya hadhara, basi wawasikilize wananchi na watekeleze ahadi walizozitoa kwa wananchi wakati wa kipindi cha kampeni, vinginevyo watarajie mabadiliko makubwa wakati wowote, wakati wa vitisho haupo tena.
“Si kweli kwamba CHADEMA tunafanya vurugu au kuchochea wananchi bali hali hiyo inasababishwa na serikali ya CCM yenyewe kutokana na kuwasababishia wananchi hali ngumu ya maisha na wananchi hao sasa wameamua kuiunga mkono ili kuelekea kwenye mabadiliko,” alisema.
Bi. Mdee alisema huko nyuma Watanzania walisoma bure kwa kutumia raslimali chache zilizokuwepo, lakini mara baada ya kuanza kuwa ufisadi elimu imekuwa ni mzigo kwa Watanzania na hata huduma za afya zimekuwa ni za matatizo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Habari wa CHADEMA Taifa, Bw. Erasto Tumbo aliwaomba Watanzania kuiunga mkono CHADEMA ili kuleta mabadiliko ya kweli hapa nchini na kwamba serikali ya CCM imekuwa ikiwajaza hofu ili waogope na iendelee kutawala nchini huko wanaotawaliwa wakihangaika kwa maisha magumu.
Aidha kwa upande mwingine aliwaomba wanaume wote kuwazuia wake zao pale wanapotaka kwenda hospitali kujifungua wasijaribu kupata Bajaj zilizoahidiwa na Rais Kikwete ambazo alidai kuwa atazileta nchini zifanye kazi ya kuwapeleka hospitali akina mama wajawazito.
“Ndugu zangu Bajaj zilizoahidiwa na Kikwete, ni hatari kwa akina mama wajawazito, pamoja na kwamba Kikwete hajatekeleza ahadi yake ya kuzileta hapa nchini, lakini nakushaurini msiwaruhusu wake zenu kubebwa na Bajaj hizo kwani ni hatari kwa maisha ya mama mjamzito,”
“Kwa kawaida Bajaj inapokuwa barabarani huwa inaruka ruka sana , sasa nielezeni kweli hapa Kikwete alitumia busara kusema ataingiza nchini Bajaj 400 kwa ajili ya kubeba wajawazito, si wote watakuwa wanafia njiani kabla ya kufikishwa hospitali kujifungua, nakuombeni hata kama atazileta, wakatazeni wake zenu wasizipande,” alieleza Bw. Tumbo.
No comments:
Post a Comment