Na Mwandishi wa EANA
WAJUMBE wa kikosi kazi cha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kinachoshughulikia sheria zinazotawala mfumo wa mawasiliano kwa njia ya kompyuta watakutana
mjini Mombasa, Kenya Jumatatu ijayo.
Mkutano huo wa siku tatu umelenga kuzungumzia uoanishaji wa sheria zinazohusu mfumo huo wa mawasiliano miongoni mwa nchi wanachama.
Mkutano huo ulioandaliwa na sekretarieti ya EAC kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (UNCTAD), pia utaangalia hatua
iliyofikiwa ya utekelezaji wa makubaliano ya awamu ya kwanza ya mchakato wa kuangalia sheria hizo , hatua iliyoidhinishwa na Baraza la Mawaziri la EAC
Novemba mwaka jana.
Aidha mkutano huo utatoa mapendekezo yake na kutengeneza rasimu nyingine ya kufanyia kazi katika awamu ya pili. Mkutano wa mwisho wa kuangalia uwezekano wa kuoanisha sheria hizo ulifanyika mjini Kigali, Rwanda Juni mwaka jana.
Awamu zote hizo zinatoa muongozo wa kutengenezwa na kutiliwa mkazo sheria hizo zilizooanishwa katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.Awamu ya kwanza inagusia uhamishaji wa fedha kielektroniki, utiaji saini wa kielektroniki na uthibitishaji wake, ulinzi wa takwimu na faragha yake, ulinzi kwa mlaji na uhalifu kwa kutumia kompyuta.
Awamu ya pili itagusia masuala kama ya haki miliki, ushindani, utozaji na
ulipaji kodi kwa njia ya kielektroniki na usahihi wa habari.
''Mkutano huo ni muhimu sana katika jitihiada za dhati ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kupambana na uharibifu and ujambazi unaofanywa kwa
kutumia teknologia ya kompyuta,'' Innocent Mungy, msemaji wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TICTRA) aliiambia Shirika huru la Habari ya Afrika
Mashariki (EANA).
Mkutano huo utahudhuriwa na wajumbe 35 wa kikosi kazi ambao wametoka ndani ya nchi wanachama na taasisi za kikanda.
“Baada ya baraza la mawaziri la EAC kukubali, nchi wanachama Burundi, Kenya, Rwanda, Tanzania na Uganda wamejiaminisha kutengeneza sheria ambnazo zinaweza kutumika katika kanda nzima,’’ kilisema chanzo cha habari cha EAC.
Haja ya kutengenezwa kwa sheria zitakazo ratibu mwenendo wa matumizi ya mfumo wa mawasiliano kwa njia ya kompyuta ilizungumzwa wakati wa mkutano wa programu ya serikali kwa njia ya elektroniki iliyoshawishiwa na sekretarieti ya EAC mwaka 2005 kama maandalizi ya mkakati wa uendeshaji wa serikali na mfumo wa biashara
kwa njia ya kielektroniki katika ngazi za kitaifa na kikanda.
No comments:
Post a Comment