Na Addolph Bruno
TIMU ya soka ya Coastal Union ya Jijini Tanga iliyopanda daraja msimu huu, inatarajia kumrejesha aliyekuwa kocha wa zamani wa timu hiyo
, Said Sheduu raia wa Kenya kukinoa kikosi hicho.
Akizungumza kwa simu jana, Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Benedict Kaguo alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya wanachama wa timu hiyo kukutana Jumapili katika makao makuu ya timu hiyo barabara ya 11.
Alisema wanachama hao wamefikia uamuzi huo kutokana na uwezo wa kocha huyo na ushirikiano mkubwa na viongozi, wakati alipokuwa akikinoa kikosi hicho misimu miwili iliyopota kabla ya kushuka daraja.
Kaguo alisema hatua ya kumsaka kocha huyo na kufikiria kumrejesha kundini, imekuja baada ya kumalizika kwa mkataba wa miezi sita wa kocha Said Ally, ambaye pia ni raia wa Kenya katika hatua ya tisa bora ya Ligi Daraja la Kwanza iliyomalizika mwezi uliopita Jijini Tanga.
Alisema kuanzia sasa uongozi wa muda uliopo madarakani, unafanya mawasiliano na kocha huyo ambapo taratibu za kumchukua zitafanyika baada ya marekebisho ya katiba yao ili iendane na ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Ofisa huyo alisema kupitia kikao hicho cha juzi tayari wamechagua kamati, ambayo itafanya kazi ya kurekebisha katiba hiyo itakayongozwa na Mwenyekiti wake Titus Bandawe, akisaidiana na Makamu wake John Lyimo na wajumbe Dkt. Ahmed Twaha, Oscar Assenga na Salim Amiri.
"Kamati hii inatarajia kupitia vifungu vya katiba ya zamani na kuongezea vipengele vipya au kupunguza panapostahili, vikiwamo vya Katibu Mkuu wa kuajiriwa, Mhazini, Ofisa Habari, ofisi, uwanja na timu ya umri wa miaka 20," alisema Kaguo.
No comments:
Post a Comment