Na Christina Gauluhanga
KUTOKUJIAMINI kwa wanawake wengi kumetajwa kuwa ni kikwazo kikubwa cha kukwamuana kwa wanawake katika harakati za maendeleo.Kutokana na
hali hiyo, wanawake viongozi, wajasilimali na wenmgine wametakiwa kujenga utamaduni wa kuwasaidia wanawake wenzao mahala popote walipo ili waweze kuinua uwezo wao kwa kuwa kila mwanamke anaweza.
Rai hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Bi. Chiku Galawa ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye hafla fupi ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani iliyoandaliwa na wafanyakazi wanawake wa Kampuni ya Business Times (BTL), inayozalisha magazeti ya Majira, Dar Leo, Spoti Starehe na Business Times.
Alisema kuwa, ni vyema wanawake wakawezeshana kwa kupeana moyo katika utendaji wa kazi na si kuendekeza mambo yasiyo na faida katika maisha.
Alisema kuwa kwa kufanya hivyo, wanawake watafikia malengo yaliyokusudiwa na kuzidi kujenga heshima ya mwanamke ambaye katika kipindi hiki anaonekana anaweza katika mambo mengi yakiwemo ya kutoa maamuzi.
"Ni nafasi yetu wanawake kutiana moyo, kusaidiana kwa hali na mali ili utendaji wa kazi uzidi kusonga mbele, lakini kwa upande wenu wanahabari jitahidini kuelimisha jamii ili iweze kumjenga mtoto wa kike katika hali ya kujiamini zaidi ambayo itamsaidia kusimama popote na kufanya kazi ya aina yoyote bila kuwa na woga," alisema Bi.Galawa.
Bi. Galawa alitumia mwanya huo kuwaonya wanawake kutokubali kutumiwa na baadhi ya watu kama daraja kwa lengo la kauwanufaisha watu wengine.
"Tusikubali kutumikishwa kwenye vitu ambavyo havina faida kwetu, wapo watu wanapenda kutumia wenzao kwa manufaa yao binafsi hivyo kila mmoja ana akili za kufikiri ni bora ukatumia muda wako kufikiri mambo yanayoweza kukuletea maendeleo," alisema Bi. Galawa.
Akizungumzia suala la uzazi wa mpango, Bi. Galawa alisema hivi sasa kuna watoto wenye umri wa miaka 12- 14 ambao wanadiriki kubeba mimba na kujikuta wakizaa watoto wenzao.
"Nina mifano mizuri tu, kwani Hospitali ya Temeke kuna watoto wadogo ambao wanazaa watoto wenzao na halii inasababisha wanashindwa kuwalea watoto hao na matokeo yake ni kuongeza idadi ya watoto wa mitaani hivyo tuna kila sababu kila mmoja kwa nafasi yake kupigia kelele hili ili limalizike ndani ya jamii yetu," alisema.
Akizungumzia maadili, alisema mama ndiye mwenye jukumu la kuhakikisha anamlea mtoto kwenye maadili yanayokubalika ndani ya jamii lakini pia kuachana na tabia ya kuwaruhusu watoto wadogo wenye umri kati ya miaka 6 hadi 7 kwenda kwenye kumbi za starehe ambako kuna vituko vya kila aina wasivyostahili kuviona.
"Hivi sasa kuna mambo mengi yanayoigwa kutoka nje ya nchi hivyo ni vema tukayatokomeza na kuacha tabia ya kuwaruhusu watoto wetu kwenda kumbi za starehe, " alisema.
Alitoa mwito kwa wanahabari wanawake kutumia taaluma yao katika kuielimisha jamii masuala mbalimbali yenye maendeleo lakini kubwa ni kujenga uwezo na kujiamini kwa wanawake ili waweze kufanya makubwa katika nchi hii.
Kwa upande wa Ofisa Utawala wa Kampuni ya Business Times (BTL), Bi. Sophia Mshangama alimshukuru mkuu huyo kwa kutembelea ofisi hizo ambapo alipata fursa ya kutoa historia fupi ya gazeti la Majira na kampuni kwa ujumla.
Alisema kuwa kampuni ina ofisi katika mikoa mbalimbali na pia imedhamiria kuongeza ufanisi wa kazi kwa kuongeza idadi ya mikoa na kujiimarisha zaidi kibiashara.
Bi. Mshangama aliwaasa wafanyakazi wanawake wa kampuni hiyo kutumia fursa wazipatazo katika kujadili changamoto mbalimbali zilizopo ndani ya jamii na mazingira wanayofanyia kazi.
"Sisi wanawake tukiwezeshwa tunaweza na si kukaa nyuma kwa kuwaachia wanaume peke yao na kuonekana hatuwezi, " alisema.
Katika sherehe hizo ambazo kilele chake huwa ni Machi 8, wanawake wa BTL husherehekea kwa kuzalisha wa gazeti la Majira ambapo wanaume huwa ni siku yao ya mapumziko.
Sherehe hizo hufanyika kila mwaka Machi 8, ambapo kimkoa itafanyika viwanja vya Zakhem Mbagala, jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment