30 March 2011

CCM yatishia kuishtaki Halmashauri Moshi

Na Martha Fataely, Moshi

TISHIO la Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutaka kukinyang’anya Chama Cha Mapinduzi (CCM) majengo na viwanja vilivyokuwa mali ya
umma, limekifanya chama hicho kikongwe kizizime na kutangaza hatua ya kuiburuza mahakamani Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kwa kuicheleweshea hatimiliki ya viwanja hivyo.

Juzi Katibu wa Madiwani wa CHADEMA, Bw. Abrahman Sharifu na mbunge wa Moshi mjini, Bw. Philemon Ndesamburo walieleza nia ya Baraza la Madiwani lililopangwa kufanyika kesho kuinyanga’anya CCM mali hizo zinazodaiwa zilikuwa za umma kabla ya mfumo wa vyama vingi. Halmashauri ya Manispaa ya Moshi inaongozwa na CHADEMA.

Kutokana na hatua hiyo, Katibu wa CCM mkoani Kilimanjaro, Bw. Stephen Kazidi alisema chama chake kinakusudia kuifikisha mahakamani manispaa hiyo na kimetoa notisi kuanzia Machi 25, ili wawe wamekamilisha taratibu za kisheria kutoa hati hizo.

Alisema Viwanja hivyo namba 056038/94 ilipo Ofisi ya CCM Moshi Mjini na kiwanja namba 15686 ilipo Ofisi ya Jumuiya ya Vijana ni mali ya CCM kwani walivipata kwa mujibu wa sheria na kuthibitishwa na vikao halali vya Manispaa ya Moshi.

Alifafanua kwamba kiwanja ilipo ofisi ya CCM Moshi mjini kilitolewa kupitia vikao halali tangu Novemba 30, mwaka 1993 na aliyekuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais kupitia barua yake namba PMO/2/U.20/18 aliridhia maamuzi ya manispaa hiyo.

Hali kadhalika Bw. Kazidi alisema kiwanja ilipo ofisi ya UVCCM kilitolewa kwa jumuiya hiyo kwa uamuzi uliofanywa na vikao vya kisheria vya halmashauri, kamati ya mipango miji, kamati ya fedha na mipango ambapo jumuiya hiyo ilitakiwa kuilipa Manispaa sh. milioni 11.7, ambazo tayari zimelipwa.

Alisema kulingana na taratibu zote zilizofuatwa majengo na viwanja hivyo ni mali ya CCM chini ya Baraza la Wadhamini wa CCM na lile la UVCCM na kwamba wataendelea kuzilinda.

Katibu huyo alisema baada ya siku 30, CCM itaifikisha Halmashauri ya manispaa ya Moshi makahamani endapo wataendelea na ubabe wa kuzuia mali halali za CCM.

Awali katibu wa Madiwani wa Chadema na diwani wa kata ya Bondeni,Bw Abrahman Sharif alisema mpango wa chama chake kuhakikisha mali hizo za umma zinarejeshwa mikononi mwa manispaa lipo pale pale kwani CCM imezipora baada ya kuwa wapangaji wa muda mrefu.

Akizungumza kwa niaba ya Bw Sharif,katibu wa Chadema mkoani Kilimanjaro,Bw Basil Lema alisema chama hicho kiliwaahidi wananchi kwamba mali hizo zitarejeshwa na ndicho kitakachofanyika Machi 31, mwaka huu.

Mkurugenzi Mtedaji wa Manispaa ya Moshi, Bi. Bernadette Kinabo alisema viwanja na majengo yanayozunumziwa na madiwani wa CHADEMA ni mali ya CCM na kwamba walipewa kihalali na Baraza la Madiwani lililopita.

Hata hivyo, kutokana na hali tete ya kikao hicho, Bi. Kinabo alisema kulingana na taarifa zilizofika ofisini kwake, kuwa madiwani CHADEMA wamewaalika wafuasi wao kwenye kikao hicho, amelazimika kuahirisha kikao cha Baraza la Madiwani kesho, kwa hofu kwamba kutatokea vurugu na umwagaji wa damu baina ya pande hizo mbili.

Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ya mwaka 1982 na marekebiso yake ya mwaka 2002, mkurugenzi amepewa mamlaka ya kuahirisha na kuitisha kikao cha Baraza la Madiwani.

6 comments:

  1. Huyu mama Kinabo ana matatizo ya ubabe ata ka yale mambo yanayoitaji hekima. Kuhairisha kikao sio tija lakini tunafahamu unavyochukulia mambo juu juu bila kuchunguza na kutafuta historia, nakusihi sana mama mkurugenzi nyakati za kuibia watanzania kwa kutumia chama chenu cha CCM ambacho vile vile ni chama changu zimeisha ila yatupasa tuwe na mtazamo na fikra chanya za kimaendeleo na maslahi ya taifa letu, kwani watanzania wa leo wameamka kutoka kwenye usingizi mzito unaofanana na madawa ya kulevya.

    ReplyDelete
  2. mama acha ubabe yanayotetewa ni maslahi ya wananchi ndio waliowachagua ili wawasaidie. baraza lililopita liliongozwa na ccm kwaio waliona kugawana ndio mpango.

    ReplyDelete
  3. nakumbuka hata mimi nilichangishwa ili kufanikisha kujenga majengo yote hayo, na hii haina maana kwambamimi nilikuwa mwanacha wa ccm, haya majengo yote inatakiwa iwe ya wananchi wote na si ya ccm

    ReplyDelete
  4. eng mwakapango, E.P.AMarch 30, 2011 at 5:05 PM

    CCM work up! imeanza moshi itakuja nchi nzima na nawakikishia hata mkiwa na mawakili wazuri kiasi gani hamwezi kushinda kesi hizo mlichangisha watanzania wote hakukuwa na itikadi yoyote kwani chama na serikali vilikuwa ni CCM TU. Hebu tukumbuke maazimio kama ya mlale ambapo ilimuliwa kila mwananchi kuchangia uwanja wa majimaji kila alyekunywa soda na bia alichangia shilingi moja kwa chupa kwa miaka mitatu na mafuta dizel na petrol vivyo hivyo acha michango ya wafanyakazi hivi unataka kuniambia hiyo ni mali ya CCM? Nenda ALI hassan Mwinyi, mapinduzi mbeya n,k nina hakika ikifika wakati watu wataandama kudai mali zao tunataka presidence hiyo ya moshi narudia kuwatafadhalisha CCM handle with care hiyo ni mali ya watanzania wote.

    ReplyDelete
  5. Ni kweli kabisa CCM hamna mali zenu , zote mlituchangisha tena kwa ubabe. Ni mali zetu! jiandaeni kuturudishia mali zetu! Watanzania tumeamka,mlikuwa mnatuibia tu! HATUDANGANYIKI TENA!

    ReplyDelete
  6. msijifarague chadema hawana nafasi nchini humo chukueni time na ukabila wenu unao wasumbua hata 2015 hamshindi hata kwa nn mna nn nyie cha kuwafanya mshinde vichaa nyie nendeni zenu tumewachoka ndugu wamiliki wa blog hizi habari za chadema au ccm ndio maendeleo kwa sasa huko tanzania?wengine tunajisikia kutapika tu kwa mambo yasio na mpango ngojeeni karne ya 200 ijayo mtapewa nchi tu hiyo

    ReplyDelete