*Ni la kuzuia wagonjwa wapya kwenda kwake
*Wabuni njia yao mpya inayokwepa vizuizi
Na Said Njuki, Arusha
WAKATI wananchi wanaokadiriwa kufikia 6,000 wakiwa wamekwama njiani kwenda kwa
Mchungaji Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Ambilikile Masapila wa Kijiji cha Samunge, Loliondo wilayani Ngorongoro baadhi watu wamepuuza agizo la serikali na ombi la mchungaji huyo, baada ya kubuni njia ya panya ili kufika kwa mchungaji huyo.
Uchunguzi uliofanywa na Majira na kuthibitishwa na baadhi ya mashuhuda umebaini watu hao wanapita barabara ya Longido, kupitia Ziwa Natron na kuibukia kijijini kwa Babu baada ya kutoa kitu kidogo.
Uchunguzi huo umebaini kuwa pamoja na kuwepo kwa ulinzi katika eneo hilo lakini ni hafifu nyakati za usiku kutokana na baadhi ya magari kupenya kutokana na wamiliki au madereva wa magari hayo kutoa kati ya sh. 20,000 hadi sh. 50,000 ili kufanikisha azma hiyo.
Tayari serikali katika kutekeleza mapendekezo ya Babu imeweka utaratibu wa vituo kwa ajili ya usajili wa wagonjwa wanaokwenda katika kijijini humo.
Vituo hivyo vipo Arusha katika Uwanja wa NMC, Babati mkoani Manyara, Mugumu na Musoma katika Mkoa wa Mara kw wale wanaotoka Kanda ya Ziwa.
“Bado shughuli ya kupenyeza wagonjwa kwenda kwa Babu linaendelea hasa kupitia Longido na Ziwa Natron na njia hiyo inawajumuisha watu wanaotoka wilaya hiyo na nchini Kenya kwa sababu kupitia Mpaka wa Namanga hali hii itachelewesha azma ya mchungaji ya kumaliza wagonjwa waliokuwa wamefika huko kabla ya Aprili Mosi mwaka huu kama alivyopanga,” alisema mmoja ya vyanzo vyetu vya habari.
Kutokana na hali hiyo baadhi ya watu waliozungumza na Majira wameiomba serikali kudhibiti njia zote muhimu ili utekelezaji wa mapendekezo ya mchungaji yawe na tija, la sivyo utekelezaji wake utakuwa mgumu hivyo kuwa sawa na kutwanga maji.
“Kumekuwepo na udhaifu wa utekelezaji wa mapendekezo kadha wa kadha kutoka hata kwa viongozi wa juu serikalini hapa nchini vivyo hivyo hata katika hili la mchungaji litakwama iwapo serikali haitakaza
kamba,” alisema Bw. John Kiwelu.
Hata hivyo, hali bado inazidi kuwa mbaya kwa wagonjwa walioziuwa huko katika vizuizi vya Mto wa Mbu na Meserani wilayani Monduli kwa kuwa sasa yamefikia magari 500 yenye watu zaidi ya 3,000.
Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Bw. Elias Wawa Lali amewatahadharisha wagonjwa wanaojiandaa kwenda kwa Babu na walio katika vizuizi mbalimbali kufuata utaratibu na kanuni zilizowekwa na Babu ili kuleta utekelezaji wenye tija kwa manufaa ya watu wote.
Akizungumza kwa njia ya simu, Bw. Lali alisema serikali haiko tayari kuwavumilia watu wanavunja utaratibu na kanuni zilizowekwa kwa faida ya wote, hivyo madereva watakaobainika kuvunja sheria hizo watakaibiliwa na adhabu kali ikiwa ni pamoja na kutoruhusiwa wagonjwa wao kupata tiba hiyo.
No comments:
Post a Comment