09 February 2011

Yanga yawaacha Nurdin, Mwasika

*Kupaa kesho kwenda Ethiopia

Na Elizabeth Mayemba

WACHEZAJI wa Yanga, Nurdin Bakari na Stephano Mwasika wamaeachwa katika kikosi cha
timu hiyo kinachotarajiwa kuondoka kesho kwenda Ethiopia.

Yanga wanatarajiwa kucheza mchezo wa marudiano michuano ya Shirikisho, dhidi ya Dedebits ya Ethiopia kati ya Jumamosi au Jumapili.

Akizungumza Dar es Salaam jana Msemaji wa klabu hiyo, Louis Sendeu alisema Nurdin anasumbuliwa na mguu wakati Mwasika anaumwa malaria, hali itakayowafanya washindwe kusafiri.

"Daktari ametaka wachezaji hawa wapewe muda zaidi wakati wakiendelea na matibabu, hivyo hatuwezi kusafiri na wachezaji ambao wanaumwa," alisema Sendeu.

Alisema kipa namba moja wa timu hiyo, Yaw Berko na beki Ernest Boakye ambao walikuwa majeruhi, wameanza mazoezi mepesi na hali zao zinaendelea vizuri ambao wana uwezekano mkubwa wakasafiri.

Sendeu alisema maandalizi ya mechi hiyo ya marudiano yanakwenda vizuri na Kocha Mkuu mpya, Sam Timbe anazidi kuwapa mbinu mpya wachezaji wake ili kuhakikisha wanashinda mchezo huo.

Alisema uongozi huo bado haujafahamu siku rasmi ya mechi yao kuchezwa na wanaendelea kufanya mawasiliano na wenyeji wao Ethiopia, kupitia Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Katika mchezo uliopita ambao ulichezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam timu hizo zilitoka sare ya mabao 4-4. Yanga wakifanikiwa kushinda mchezo huo, raundi inayofuata watakutana na El- Al Hadoud ya Misri.

No comments:

Post a Comment