03 February 2011

Yanga yakwaa kisiki

*Yapigwa bao 1 na Mtibwa

Na Zahoro Mlanzi

VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga jana ilikwaa kisiki baada ya kufungwa bao 1-0 na Mtibwa Sugar katika
mechi ya ligi hiyo iliyopigwa Uwanja wa uhuru, Dar es Salaam.

Mtibwa ilipa bao hilo dakika ya 70 kupitia kwa Hussein Java, aliyechukua nafasi ya Mgwao, baada ya kuunganisha krosi ya Juma Abdul. 

Katika mechi hiyo Yanga, ndiyo ilikuwa ya kwanza klubisha hodi katika lango la Mtibwa baada ya David Mwepe na Jerison Tegete kushindwa kufunga katika dakika ya kwanza wakiwa ndani ya eneo la hatari.

Mtibwa walijibu mashambulizi ya nguvu ambapo dakika ya 15, Omari Matuta kupiga kichwa kilichotoka nje baada ya kuunganisha krosi ya Yusuf Mgwao huku Julius Mrope akikosa bao baada ya kubaki na kipa lakini akashindwa kuitumia nafasi hiyo.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kushambuliana kwa zamu ambapo katika dakika ya 52, Nurdin nusura aifungie timu bao lakini mpira wa kichwa alioupiga ulitoka nje ya lango.

Mtibwa nayo ilijibu shambulizi hilo dakika ya 54, ambapo mshambuliaji wake Omari Matuta alishindwa kupachika mpira wavuni baada ya kutoa mpira nje akiwa na kipa.

Dakika ya 61, Juma Abdul wa Mtibwa alikwamisha mpira wavuni, lakini hata hivyo bao hilo lilikataliwa na mwamuzi wa mchezo huo alilikataa kwa madai kwamba mfungaji kabla ya kufunga alikuwa ameotea.

Kwa matokeo hayo Yanga bado ipo kileleni kwa kuwa na pointi 31, ikifuatiwa na Simba yenye pointi 27 huku Mtibwa Sugar na Azam FC zikifungana kwa pointi 26 lakini Azam inaongoza kwa tofuati ya mabao ya kufunga.

Mechi nyingine ya ligi hiyo, inatarajia kuendelea tena leo katika uwanja huo ambapo mabingwa watetezi, Simba wataumana na African Lyon ambayo ipo katika nafasi ya nane katika msimamo wa ligi.

No comments:

Post a Comment