SERIKALI kupitia Kituo chake cha Uwekezaji nchini (TIC), imekuwa ikifanya jitihada kubwa za kutoa elimu ya maarifa kwa wajasiriamali wadogo na wale wa kati ili waweze kukuza mitaji yao, kujiendeleza kibiashara na kufikia malengo.
Hivi karibuni, TIC kilitoa mafunzo kwa wajasiliamali zaidi ya 30 kutoka mikoa ya Kilimanjaro na Arusha ili waweze kufanya biashara na wawekezaji wakubwa wa ndani na nje ya nchi.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho Bw. Raymond Mbilinyi, alisema programu hiyo ilianza mwaka 2009 ambapo hadi sasa jumla ya wajasiliamali 250 wamenufaika na mafunzo hayo na mafanikio yameanza kuonekana.
Alisema kituo hicho kimekuwa na utamaduni wa kuwatembelea wajasiliamali hao katika maeneo wanayofanyia biashara ili kuona jinsi wanavyotekeleza kwa vitendo kile walichofundishwa.
Sisi tunasema kuwa, mafunzo hayo yana umuhimu mkubwa kwa TIC, wajasiliamali wenyewe na Taifa kwa ujumla kwani lengo ni kuwaunganisha na wawekezaji wakubwa na kukuza kipato chao.
Ukweli ni kwamba, Tanzania haiwezi kuendelea na kupiga hatua inayotazamiwa na wengi kama Serikali yao itashindwa kuelekeza nguvu zake kwa kuwaendeleza wajasiriamali wadogo na kati.
Mpango huo utawasaidia wajasiliamali hao kuwa wakubwa, kuanzisha viwanda vyao na kutoa ajira kwa Watanzania ambao watashiriki katika harakati za ukuaji uchumi.
Ripoti ya hali ya uwezekaji nchini, inahimiza wajasiriamali wa ndani wawekewe mazingira mazuri ya biashara ili waweze kukua na kushiriki katika harakati za kupiga vita umaskini
Kimsingi wajasiliamali wengi wadogo na wale wa kati, hawajawekewa mazingira mazuri ya kushiriki kwenye shughuli za kukuza uchumi na kuharakisha maendeleo.
Umefika wakati wa Serikali kuweka dhamira ya kweli ili kulisaidia kundi hili kwa kuhakikisha inaweka sera maalumu ambayo itawawezesha kupata mikopo nafuu.
Mikopo hiyo ni ile inayotolewa na benki mbalimbali nchini, vinginevyo Tanzania itazidi kubaki nyuma.
No comments:
Post a Comment