23 February 2011

Yanga watoa msaada Gongolamboto

 Na Elizabeth Mayemba

WACHEZAJI wa Yanga, jana waliwakumbuka waathirika wa mabomu ya Gongolamboto, Dar es Salaam kwa kuwapelekea msaada wa vifaa mbalimbali vikiwemo
maji, sabuni na kalamu (peni).

Akikabidhi vifaa hivyo nahodha wa timu hiyo, Fredy Mbuna alisema wameguswa na tukio hilo la kuhuzunisha na ndiyo maana wakaona hawana budi kuwachangia kitu kidogo walichonacho kama wachezaji.

"Wakati janga hili linatokea tulikuwa Bukoba kwenye mchezo wetu na Kagera Sugar, hivyo tukaahidi kwamba tutakaporejea Dar es Salaam tutakuja kuwapa pole waathirika wa mabomu na kutoa kile tulichonacho kama wachezaji," alisema Mbuna.

Alisema siku zote wataendelea kuwakumbuka waathirika hao na wakipata chochote tena, hawatasita kwenda kuwasaidia.

Mbuna alisema kuwa hata mchezaji mwenzao, Godfrey Bonny ni mkazi wa Gongolamboto, hivyo endapo angekuwepo huenda adha hiyo ingemkuta.

Katika hatua nyingine, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo Mohammed Bhinda, alisema msaada huo ambao umetolewa ni wachezaji wenyewe ndiyo walioamua kufanya hivyo kwa jinsi walivyoguswa na janga hilo.

Alisema viongozi nao watapanga siku maalum kwa ajili ya kwenda kutoa pole kama walivyofanya wachezaji wao.

"Wachezaji wetu waliahidi kwamba wakitoka Bukoba watakwenda kuwapa pole waathirika wa mabomu na sisi tukawapa baraka zote, kwani kitendo walichokifanya ni cha ubinadamu," alisema Bhinda.

1 comment:

  1. Hongereni sana sana wachezaji wa Yanga, kwa hilo mmewapiga bao wachezaji wa timu nyingine zote! Mungu awabariki mchukue ubingwa wa Tz!

    ReplyDelete