28 February 2011

...Yanga waivamia kambini

Na Mwandishi Wetu

ZIKIWA zimebaki siku sita kabla ya mchezo wa watani wa jadi Ligi Kuu, Simba na Yanga kuumana, tayari vituko vimeshaanza ambapo viongozi wa
Yanga jana wamevamia kambi ya Simba iliyopo katika hosteli ya Lamada Dar es Salaam.

Simba iliingia katika kambi hiyo, wiki iliyopita kwa ajili ya kujiandaa na michuano mbalimbali ikiwemo ya Ligi Kuu, pamoja na mechi ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya TP Mazembe.

Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika kutoka hotelini hapo Dar es Salaam jana, kililiambia gazeti hili kwamba baadhi ya viongozi wa Yanga walionekana hotelini hapo wakifanya kikao chao cha Kamati ya Utendaji cha kujadili mambo mbalimbali likiwemo suala la mdhamini wao, Yusuf Manji ambaye alitangaza kujiondoa katika klabu hiyo.

"Tulishaanza kuwazoea Simba ambao wapo hapa kama wiki sasa lakini leo hii (jana), tunashangaa kuwaona viongozi wa Yanga nao wakija hapa tulipojaribu kuuliza tukaambiwa wana kikao cha Kamati ya Utendaji ambacho walipanga kufanyia hapa," kilisema chanzo hicho.

Kiliendelea kusema kuwa hali hiyo ya kuonekana kwa viongozi wa Yanga katika kambi ya Simba, ilitia hofu kubwa hata kwa baadhi ya wanachama wa Simba, waliokuwepo kambini hapo kuangalia mwenendo wa kambi hiyo.

Akizungumzia hali hiyo, Meneja wa Simba Innocent Njovu alisema kwamba viongozi hao hawana madhara yoyote kwao na pia wana haki ya kukutana popote nchini.

"Ni kweli tumewaona viongozi wa Yanga hapa, lakini nimesikia wao wana kikao chao cha Kamati ya Utendaji, kitu ambacho sisi hakitutii hofu yoyote ile," alisema Njovu.

Alisema wao kwa sasa nguvu zao wamezielekeza katika mechi zote zinazowakabili, hivyo hawatakaa kuwafikiria wapinzani wao Yanga wanachokifanya.

Nao viongozi wa Yanga, walipotafutwa kuzungumzia hali hiyo hawakuweza kupatikana baada ya simu zao za mkononi kuwa zimezimwa.

1 comment:

  1. Utoto huo! ina maana mpira wetu hauendi mbele bila ya hongo? Yanga na simba zimekuwapo, zimehongana, washabiki wametwangana na mpira hauendelei. Timu ziwekeze katika kuzijenga badala ya kubaki na fikra mgando eti wamekwenda kuloga ama kuhonga timu. Tafakarini kwa makini

    ReplyDelete