Na Mwandishi Wetu, Moshi
MBIO za Tisa za Kimataifa za Kilimanjaro Marathon zimerindima mjini hapa huku ikishuhudiwa Watanzania watatu pekee Banuelia Brighton, Mary Naali na
Stephen Huche wakiingia tatu bora mbele ya Wakenya ambao walitawala vilivyo mbio hizo.
Banuelia ambaye ndiye anashikilia rekodi ya taifa ya Marathoni kamili kwa wanawake, aliibuka nafasi ya pili katika mbio hizo za kilomita 42, akitumia saa 3: 02.52 akitanguliwa na mshindi wa kwanza Anna Kamau aliyetumia saa 3:00.16 kutoka Kenya huku nafasi ya tatu ikienda kwa Mkenya mwingine Ophra Oruke 3:03.20.
Machungu yaliwazidi Watanzania mbele ya mgeni rasmi, Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Emmanuel Nchimbi, pale kwa upande wa wanaume ambako nafasi ya kwanza ilikwenda kwa Mkenya Kipkemboi Kipsang aliyetumia saa 2: 17.08 akifuatiwa na Julius Kilimo 2:17.10 huku nafasi ya pili ikinyakuliwa mwanariadha anayechipukia nchini Steven Huche saa 2:19.24.
Katika Nusu Marathoni wanawake Valentine Kipketer aliibuka kidedea akitumia saa 1:15.08 akifuatiwa na Loren Kitita 1:15.48 wote kutoka Kenya huku Mtanzania Mary Naali akikamata nafasi ya tatu kwa saa 1:15.55.
Kwa wanaume Michael Kemau aliibuka mshindi wa kwanza akitumia saa 1:03.58 akifuatiwa na Leonard Muchare huku nafasi ya tatu ikienda kwa Geofrey Ndungu saa 1:04.04 wote kutoka Kenya.
Washindi katika mbio hizo walizawadiwa zawadi na Waziri Nchimbi ambaye mbali ya kuwashukuru waandaaji kwa kumualika pia alitoa shukrani za pekee kwa wadhamini wakuu wa mbio hizo bia ya Kilimanjaro Lager na wadhamini shirikishi kwa mchango wao katika kukuza mchezo wa riadha.
Alisema, jitihada zao za kuwekeza rasilimali na fedha katika mbio hizo zimeleta faida kubwa kwa kuwapa fursa wanariadha wa Tanzania kujipima na wanariadha wa kimataifa na hatimaye kukuza viwango.
Alisisitiza kuwa, kufanya vyema kwa wanamichezo wa hapa nchini kimataifa kunawapa raha Watanzania, jambo ambalo ni muhimu kwani linawafanya kufurahi na kusahau matatizo yao ya kawaida.
Kwa upande wake Meneja Mawasiliano wa TBL, Emmy Oriyo alisema, kwa kuwa mwaka kesho mbio hizo zinatimiza mwaka wa 10 tangu kuanzishwa kwake, Kilimanjaro Premium Lager inatoa ahadi kwamba itawekeza zaidi katika mbio hizo, ili kuhakikisha maadhimisho ya kumi yanakuja na ongezeko la zawadi na udhamini mkubwa zaidi katika maeneo mengine yote.
Kwa upande wa burudani bendi ya The African Stars Entertainment ‘Twanga Pepeta’ TMK Wanaume Family na Joseph Payne ‘Mzungu wa BSS’ walipagawisha vilivyo.
Mbio hizo zimedhaminiwa na bia ya Kilimanjaro ambao ndiyo wadhamini wakuu, Vodacom Tanzania (mbio za kujifurahisha), DT Dobie, TPC Sugar, Kilimanjaro Water, Tanzanite One, Simba Cement, Keys Hotel, Tanzanite One, Precisionair, KK Security na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), huku waratibu wakiwa ni Wild Frontiers ya Afrika Kusini na Executive Solution ya Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment