25 February 2011

Viongozi wawe na ukomo wa madaraka

Na Faida Muyomba, Geita

NCHI za bara la Afrika zimetakiwa kuwa na muda maalumu wa ukomo wa madaraka ili kuepuka kuzuka kwa migogoro na machafuko yanayoweza
kusababisha maafa.

Askofu Mkuu Kanisa la African Inland Church of Tanzania(AICT), Jimbo la Geita, Bw. Mussa Magwesela alitoa kauli hiyo katika mazungumzo maalumu na Majira, yaliyofanyika ofisini kwake jana.

Majira lilitaka maoni yake kuhusiana na kuwepo kwa wimbi la machafuko kadhaa kwa baadhi ya nchi za bara la Afrika Kaskazini ambako wananchi kuandamana kwa kuwakataa viongozi wao.

Alisema mfumo wa uongozi kwa nchi nyingi za bara la Afrika, umejaa udikiteta jambo ambalo limesababisha wananchi kutokubaliana nao hivyo kuhitaji uhuru wa kidemokrasia.

"Ukiangalia nchi nyingi ambazo zina migogoro kama vile Ivory Coast, Libya na nyinginezo utabaini kuwa hawana mfumo mzuri wa uongozi hasa kwa ngazi ya urais, siyo mzuri kwani baadhi zimetokana na katiba dhaifu walizojiwekea. Rais anaweza kuwa madarakani zaidi ya miaka 20 hii ni hatari kabisa, ni bora rais atawale kipindi cha miaka minne hadi 10 tu basi, alisema.

Alisema, kutokana na mfumo huo, katiba inampa mamlaka makubwa zaidi rais wa nchi kusema chochote anachotaka, kutenda jambo lolote bila kuulizwa hata kama litakuwa na madhara kwa wananchi anaowaongoza.

Alisema kuwepo kwa mfumo madhubuti wa uongozi kutaondoa utata unaozikabili nchi hizo hasa kutokana na kuwepo kundi kubwa la vijana ambalo halikubaliani na viongozi wanaokaa madarakani kwa muda mrefu kwa vile hawana faida nao.

Alisema asiyekosea ni Mungu pekee, hivyo kutaka viongozi wanapokosea, jamii iwe na uweoz wa kuwawajibisha kwa makosa yao.

No comments:

Post a Comment