Na Elizabeth Mayemba
KAMATI ya Utendaji ya Yanga, itakutana keshokutwa kupanga tarehe ya Mkutano Mkuu ulioombwa na Wanachama wa klabu hiyo.Akizungumza Dar es Salaam
jana Msemaji wa Yanga, Louis Sendeu alisema kamati hiyo imeamua kukutana keshokutwa baada ya Jumanne kushindikana kwa sababu baadhi ya viongozi hawakuwepo.
"Keshokutwa Kamati ya Utendaji itakutana kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali na ajenda kubwa itakuwa ni ile ya kupanga tarehe ya Mkutano Mkuu wa Wanachama," alisema Sendeu.
Alisema Jumanne walishindwa kukutana kwa sababu Mwenyekiti, Lloyd Nchunga na Makamu wake Davis Mosha, walikuwa safarini pamoja na baadhi ya wajumbe wengine, hivyo mpaka kufikia keshokutwa endapo kolamu ya wajumbe itatimia watafanya kikao hicho.
Hivi karibuni baadhi ya wanachama wa klabu hiyo, waliuomba uongozi wa Yanga kuitisha haraka Mkutano Mkuu wa dharura kwa lengo la kujadili mambo mbalimbali lokiwemo la kutoelewana baina viongozi.
Katika hatua nyingine, Sendeu alisema timu yake inaendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Kaunda uliopo makao makuu ya klabu hiyo mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam chini ya kocha wake Mganda Sam Timbe.
Sendeu alisema wanajindaa na mchezo wao wa Jumatatu, dhidi ya Ruvu Shooting utakaochezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
No comments:
Post a Comment