03 February 2011

Shule binafsi hawana hoja-NECTA

Na Mwandishi Wetu

BARAZA la Mitihani Tanzania (NECTA) limesema kuwa madai ya Chama cha wamiliki na mameneja wa shule na vyuo visivyo vya
serikali (TAM0NGSCO) ya kutoridhishwa na usahihishaji wa mitihani ya kidato cha nne hayana msingi kwa kuwa taratibu zote zilizingatiwa.

Akizungumza na Majira kwa simu jana, Katibu Mtendaji wa NECTA, Dkt. Joyce Ndalichako alisema pamoja na uhuru wa maoni wa wamiliki hao, hoja zao hazikufanyiwa kazi ya kutosha hivyo kukosa usahihi.

Dkt. Ndalichako alikuwa akijibu madai ya wamiliki hao waliotaka matokeo ya mitihani ya kidato cha nne 2010 yafutwe na mtihani usahihishwe upya kwa sababu hawakuridhishwa na utaratibu uliotumika katika usahihishaji.

Kwa mujibu wa chama hicho usahihishaji wa mtihani kwa mwaka jana haukuwa mzuri kwa sababu ulichukua muda mfupi kutokana na bajeti ya baraza la mitihani kuwa ndogo.

Lakini Dkt. Ndalichako alisema hakukuwa na upungufu wowote wa bajeti kwa kuwa serikali iligharamia shughuli nzima ya kusahihisha mitihani kwa asilimia 100, na kwa kuzingatia ongezeko la watahiniwa mwaka 2010 ukizinganishwa na mwaka uliotangulia.

Alisema muda waliodai kuwa ni mfupi kusahihisha mitihani hiyo haukuwa na tofauti na uliotumika mwaka 2009, na kuwa NECTA ilipanga walimu wa wengi zaidi wa kusahihisha kwa kuzingatia idadi ya wanafunzi waliotahiniwa.

"Mwaka 2009 tulikuwa na makers (wasahihishaji) 3,054 na mwaka jana tuliongeza idadi hadi 4,546 ili kukidhi ongezeko la wanafunzi, hivyo hatukuwa na upungufu na uliotumika ulikuwa sawa sawa," alisema Dkt. Ndalichako.

Dkt. Ndalichako alitoa mfano wa somo la Kiswahili lililochukua muda mrefu kusahihishwa kuwa lilitumia siku 32, walimu 293 mwaka 2009; na mwaka jana likatumia siku 36, walimu 539.

"Kwa hiyo hapo utaona kuwa tulizingatia ongezeko la wanafunzi, tukaongeza wasahihishaji na siku zilikaongezeka. Kwa masomo mengine siku zinatofautiana kulingana na idadi ya watahiniwa na walimu tuliopanga," alisema.

Kuhusu madai kuwa ufaulu mdogo umechangiwa na mtaala mpya, Dkt. Ndalichako alisema ni kweli mtaala ni mpya, lakini hoja hiyo haina ukweli kwa kuwa mkupuo wa kwanza kuhitimu chini ya mtaala huo ni mwaka 2008, hivyo isingekuwa rahisi matokeo mabaya yakawakuta tu wanafunzi wa 2010, miaka mitatu baadaye.

Alipoulizwa sababu za ufaulu mdogo mwaka 2010, alisema yeye hayuko shuleni hivi sasa, lakini kwa ujumla ufaulu unategemea kuwapo kwa walimu wanaojituma kufundisha, wanafunzi wenye ari ya kujifunza na mazingira mazuri ya shule.

"Siwezi kusema moja kwa moja nini kimetokea huku shuleni kwa kuwa mimi sipo huko, na sijafanya uwiano wa kuangalia nani amefaulu au kufeli na kwa sababu gani," alisema.

4 comments:

  1. Kuferi kumetokana na ongezeko la shule za kata ambazo zina mazingira mabaya ya kusomea, lakini hata hivyo watoto kitendo cha kukaa shuleni miaka miine ni elimu tosha, huwezi kulinganisha na mtoto ambaye hajaenda sekondari kabisa, so wazazi msifikiri kuwa kwa kuwa mwanenu kapata zero hana kitu. la hasha! he/she can do better in life than those who scored the first division. Kuvujika kwa mpini siyo mwisho wa kilimo.

    ReplyDelete
  2. Binadamu siku zote hatuna kheri!! ilikuwa tunalalamika shule hazitoshi,leo shule zimejaa kila kata lakini leo zinabezwa hizo shule za kata,wazazi tuangalie tatizo kwa nini walimu hawajitumi, tuangalie posho zao,makazi yao na vitendea kazi twende mbele sio tunalaumu eti utitiri wa shule za kata ndio umesababisha kufeli sio kweli,muhimu watoto wetu pia tuwakaguwe vitabu vyao sio tunawaachia uhuru watakavyo,nia ya shule za kata pia kuwa wanafunzi wasome na mahali waishipo hasa ukizingatia tatizo la usafiri dar wazazi tunakubali mtoto akasome kunduchi wakati unakaa gongo la mboto au mbagala au kigamboni, anatoka alfajiri anarudi usiku hivi unategemea nini? anakuwa hana hata muda wa kujisomea tubadilike sio kila kosa tunaisukumia serikali mengine tuna uwezo nayo wenyewe wazazi

    ReplyDelete
  3. Jamani watanzania kuna mambo mengi sana yamechangia kuwepo kwa matokeo mabovu ya kidato cha nne. Baadhi ya sababu ni kama zifuatazo.

    1) Uaba wa walimu hasa katika shule za kata, huaba huo umesababisha hata baadhi ya wanafunzi kupoteza mori wa kusoma.

    2) Kufutwa kwa mtihani wa kitaifa wa kidato cha pili, imesababisha baadhi ya wanafunzi kutokua na munkari wa kusoma.

    3) Mazingira mobovu ya kusomea, ikiwa ni pamoja na ukosefu wa maabara, vitabu vya kujisomea,

    4) Uzoefu wa waalimu, Walimu wengi wapya walioajiriwa na serikali katika shule mpya za kata wengi hawana uzoefu na kazi, na kuna baadhi ya shule waaalimu wakidato cha nne nimara yao ya kwanza kufundisha.

    Kwa hiyo watanzania, wasitumie muda huu kurushiana mpira, ni wakati wa kuangalia namna ya kuboresha elimu, ili tuweze kupata hapo baadae wataalamu wenye sifa wa kuitumikia nchi. Katika hili unahitajika ushirikiano wa wazazi, walimu, wadau mbalimbali wa elimu pamoja na serikali.

    ReplyDelete
  4. Tatizo ni wasimamizi wa wajuu elimu. Wasikwepe majukumu yao. Kufeli watoto kwa kiasi hiki inamaana shule za kata ndio zimeanza jana?

    Mbona kwenye shule zingine za zamani pia wamefeli?

    Tupeni sababu za maana kama watu mlioenda shule. Sio kuja na majibu ya haraka haraka kuwa bajeti ilikuwa sawa na ya mwaka jana. So what? Tupe sasa sababu kwa nini watoto wamefeli.

    Wale mnaosingizia wazazi au waalimu sio kweli. Waalimu ni walewale na wazazi ni walewale wa mwaka jana kama bajeti anayodai mheshimiwa. Tuambieni kama hawa wanafunzi walifundishwa na waalimu wapia au kama wanafunzi wote ni wa wazazi wanaooanza kusomesha.

    Fanyeni utafiti wa kisayansi, utupe na data zinazotoa ushahidi kujenga hoja yako dkt. Ndalichako.

    Haya mambo ya kutokuwa makini kwenye maisha ya watanzania tumeyachoka. Kama una uhakika na kazi yako ya kusahihisha, waonyeshe hao wenzako data ya mambo yalivyokuwa ili wajue tatizo limetokea wapi. sio kusema tu hoja zao hazina nguvu, ili tuseme zako zina nguvu?

    Tunajua sio kazi yako kufundisha, ila sema wapi kulikuwa na mapungufu kulingana na mlivyoona na kwa sababu gani wanafunzi walifeli.

    Haiwezekani shule zote wafeli. Sio shule zote ni mpya. kama ni za kata tu ndio wamefeli tuambie, wanafunzi wa shule za kata ni asilimia ngapi ya wanafunzi wote? wanafunzi wa kata wamefeli kwa asilimia ngapi na wanafunzi wa shule zingine wamefaulu kwa asilimia ngapi?

    ReplyDelete