Na Amina Athumani
CHAMA Cha Riadha Tanzania (RT), kimetangaza nchi 10 zitakazoshiriki mashindano ya riadha ya Afrika Mashariki na Kati, yatakayofanyika Dar es Salaam
Juni 3 mwaka huu katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Nchi hizo ni Misri, Jubouti, Elitrea, Somalia, Ethiopia, Sudani, Kenya, Uganda, Zanzibar na Tanzania Bara.
AKizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa RT, Suleiman Nyambui alisema kuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la riadha Afrika Mashariki na Kati amepewa jukumu la kuhakikisha mialiko yote inafika kwa mashirikisho ya riadha ya nchi hizo na kuhakikisha zinathibitisha ushiriki wao.
"Kikao cha Kamati ya Utendaji kimeandika barua za mialiko kwa nchi 10, ambazo ndizo zitakazoshiriki mashindano haya, ambayo yanafanyika Tanzania kwa miaka miwili mfululizo hivyo tayari RT, tumeshakutana na tunaanza maandalizi mapema," alisema Nyambui.
Alisema RT imepewa kibali cha kuandaa mashindano hayo kwa miaka miwili mfululizo, baada ya kuandaa mashindano kama hayo yaliyofanyika mwaka jana na kwamba Shirikisho la Riadha Afrika Mashariki na Kati, limeridhishwa na ubora wa Uwanja wa Taifa hivyo kuwataka RT kuwa tena wenyeji wa michuano hiyo.
Nyambui alisema mashindano hayo yatashirikisha wanariadha wakubwa na wakongwe tofauti na ya mwaka jana ambayo yalishirikisha vijana chini ya miaka 17 na Zanzibar, ikaibuka washindi wa jumla wa michuano hiyo.
No comments:
Post a Comment