04 February 2011

Real Madrid, Barcelona kukutana fainali

MADRID, Hispania 

TIMU ya soka ya Real Madrid itakutana na wapinzani wao wakubwa Barcelona katika mechi ya fainali ya Kombe la Mfalme Aprili mwaka huu.Miamba
hiyo ya Hispania inakutana, baada ya Real Madrid inayonolewa na kocha, Jose Mourinho kuwafunga mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Sevilla mabao 2-0 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu.

Ushindi huo unaifanya Real Madrid kutinga hatua hiyo ya fainali kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2004.

Katika mechi hiyo ambayo ilifanyika usiku wa kuamkia jana, mshambuliaji mpya wa timu hiyo raia wa Togo, Emmanuel Adebayor ndiye aliyeifungia Real Madrid bao la kwanza na likiwa ni la kwanza kwake tangu ajiunge na timu hiyo katika muda wa nyongeza, huku bao hilo likiwa ni la pili baada ya Mesut Ozil, kuipatia bao dakika ya 81 na kuifanya timu hiyo kusonga mbele kwa jumla ya mabao 3-0.

Kocha huyo Mreno kwa sasa anakuwa na nafasi ya kutwaa taji lake la kwanza, akiwa na klabu hiyo na ambalo litakuwa ni Kombe la kwanza la Mfalme kunyakuliwa na timu hiyo, tangu mwaka  1993.

Matokeo hayo yanavifanya vigogo hivyo vya soka nchini Hispania, kukutana katika hatua hiyo ya fainali huku kocha Mourinho, akiwa na matumaini ya kufanya vizuri tofauti na ilivyokuwa kwenye mechi ya ligi ambapo timu yake ilifungwa mabao 5-0 na Barcelona kwenye Uwanja wa  Camp Nou.

Kwa upande wake Barcelona, wao wamefanikiwa kutinga hatua hiyo baada ya kuilaza Almeria mabao 3-0, hivyo kusonga mbele kwa jumla ya mabao 8-0.

Miamba hiyo ya soka inatarajia kukutana Aprili 20 mwaka huu zikiwa ni siku nne baada ya kukutana kwenye michuano ya ligi.

No comments:

Post a Comment