08 February 2011

Mlimani wamtoa jasho Kawambwa

*Wenzao Moshi wagoma kuwaunga mkono

Tumaini Makene, Dar na Martha Fataely, Moshi

PATASHIKA ya mgomo wa wanafunzi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) imeendelea kushika kasi, huku wakilazimika kutoana jasho na
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Bw. Shukuru Kawambwa, juani kwa takribani masaa 2 bila kufikia mwafaka, huku askari polisi nao wakirusha mabomu ya machozi dhidi ya mawe na chupa za maji.

Mgomo huo wa wanafunzi wa UDSM ambao ulianza kama maandamano ya amani juma lililopita, wakidai nyongeza ya fedha za chakula na malazi iwe sh. 10,000 kutoka 5,000 ya sasa umeingia hatua nyingine, wakidai kuwa hawako tayari kurudi madarasani wala kuona chuo hicho kikifungwa.

Patashika ya jana ilianza mapema mnamo saa 2 asubuhi, ambapo wanafunzi walijihimu kumsubiri Dkt. Kawambwa ambaye taarifa za awali zilisema kuwa angekuja saa 4 kuzungumza nao, lakini kadri muda ulivyokuwa ukiwadia, hakukuwa na dalili za waziri huyo kutokea.

Huku wakiamua kubadilisha eneo la mazungumzo hayo, ambalo kabla ilipangwa yafanyike katika ukumbi maarufu kwa mihadhara chuoni hapo wa Nkrumah, wakisema kuwa hautoshi kwani kila mtu alikuwa na hamu ya kumsikia waziri atakachokisema, hivyo lilihamishiwa katika viwanja vinavyotumika kwa ajili ya michezo mbalimbali chuoni hapo.

Saa 4 ilitimia bila Dkt. Kawambwa kuonekana, wala wanafunzi kuwa na taarifa yoyote juu ya ujio wake, kitendo kilichoaanza kuwapandisha mori, wakianza kuhisiana usaliti miongoni mwao, kwa kitendo cha wengine kutangulia viwanjani lakini wengine wakabaki wakizagaa eneo la Nkrumah.

Huku wakiimba nyimbo na kusema misemo ya kuhamasishana kama vile 'Revolution...for changes'...'solidarity forever' wakaamua kujipanga upya na kufanya maandamano ya amani kutoka mti maarufu wa 'Mdigrii' uliopo katikati ya chuo, wakipitia eneo la utawala, kuelekea uwanjani kumsubiri Dkt. Kawambwa.

Uwanjani, kabla waziri hajawasili, shughuli pekee ilikuwa ni kuimba nyimbo mbalimbali, ukiwemo wimbo wa taifa, wimbo wa kumbukumbu kwa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, wakisema kama si juhudi zake, viongozi walioko madarakani sasa, 'wasingesoma bure'.

Robo saa kabla waziri hajafika uwanjani, zilitangulia magari manne yakiwa yamejaa Askari wa Kutuliza Gashia (FFU), ambapo wanafunzi hao waliwazomea, baadhi yao wakisema 'hakuna fujo hapa, hapa tunajenga hoja, hapa ni chuo kikuu', baada ya takribani dakika 10, polisi wale waliondoka katikati ya uwanja wa mazungumzo na kuegesha magari mbali kidogo, tayari kwa lolote.

Ilipotimu saa 7.00 Dkt. Kawambwa aliwasili, akisindikizwa na Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Rwekaza Mukandala, Naibu Makamu Mkuu wa UDSM, (Taaluma) Prof. Makenya Maboko, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo Ustadi, Prof. Hamis Dihenga na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Bw. Charles Kenyela, huku msafara huo ukitanguliwa na pikipiki ya polisi.

Shughuli ya kutoana jasho, kwa maswali na majibu, kushangilia, kuzomea, kutoa hoja na kujibu hoja, huku waziri akipewa angalizo "Shukuru Kawambwa hatutaki uongee siasa', zilianza kwenye jua kali la mchana, kwa Prof. Mkandala kumkaribisha 'mgeni rasmi'.

"Mheshimiwa waziri karibu mbele yako ni wanafunzi wetu ambao wana masuala yanayowasibu, hivyo walisema wanataka msimamo au majibu ya serikali kutoka kwa waziri mhusika wa elimu, karibu ingawa jua ni kali, uzungumze nao," alisema Prof. Mkandala ambaye awali wakati akiwasilimia kwa kusema 'habari zenu', wanafunzi walijibu 'mbaya! mbaya! mbaya!', naye akasema "najua ni mbaya lakini tusikilizane."

Dkt. Kawambwa alianza kwa kuwataka wawe wavumilivu na wasikivu, huku akitaka kujua hoja zao za msingi katika mgomo wao huo, ili ajibu moja baada ya nyingine, akisisitiza kuwa hatazungumza siasa kama walivyotoa rai mapema, kwa maneno na katika mabango yao mengi.

"Sasa tuongee mambo...tuongee issues on the ground (uhalisia wa mambo yanayojiri), tuache siasa, mtambue kuwa mimi sikuzuka tu kuwa waziri, nilikuwa pale (akionesha Chuo Kishiriki cha Injinia na Teknolojia, CoET), jengo langu lile pale, mimi ni mwenzenu, sio kwamba nazungumza vitu ambavyo kama vile mimi sijawahi kuwa kama ninyi.

"Nipeni issues zenu hapa, nini hasa hoja zenu...," alisema Dkt. Kawambwa huku mwanafunzi mmoja aitwaye Richard Mwita, akijitokeza na kumwambia "hoja ya wananchi hawa (wanafunzi) ni kuongezwa kwa fedha za kujikimu, kutoka sh. 5,000 mpaka sh. 10,000, utuambie kwa maandishi, tunazipataje na lini."

Hoja nyingine mbili zilizoibuliwa katika mazungumzo hayo, zilikuwa ni madai kuwa wanafunzi sasa wameishiwa kabisa fedha za kuwafikisha mwisho wa 'semester' kwa siku 35 zilizobaki, hivyo serikali iangalie utaratibu wa kuwapatia walau sh. 100,000 kwa kila mmoja.

Pia wakataka wenzao waliokamatwa na kisha kufunguliwa mashtaka katika maandamano ya amani waliyofanya Ijumaa, juma lililopita, waachiwe bila masharti na kesi waliyofunguliwa ifutwe.

Akijibu, alisema, "Juu ya hoja ya kwanza ya kuwa hamna fedha na walau kila mwanafunzi apatiwe shilingi laki moja, hilo haliwezekani...mmesema tusiongee siasa...hilo haliwezekani, maana hapa nazungumza na wanafunzi wote wa elimu ya juu, piga hesabu ya fedha hizo kwa idadi ya wanafunzi wote nchini ambao ni elfu tisini na nne na mia nne thelathini.

"Hilo haiwezekani pesa kupatikana leo kama mnavyosema, siasa sasa pembeni tunazungumzia mambo ya mfukoni, si vizuri waziri kuzungumzia kisichowezekana...suala la pili nimeshaangiza mamlaka za polisi ziwaachie kwa dhamana...hilo la kesi kufutwa ni suala la mhimili mwingine wa mahakama, siwezi kulisemea.

"Suala la tatu, mmekusanyika hapa mnataka kuongezwa kwa posho ya malazi na chakula, kutoka shilingi elfu tano mpaka elfu kumi, naomba niwaambie serikali inakusudia kuongeza hiyo posho yenu, lakini shilingi ngapi ni mpaka hazina ifanye mahesabu, kima hicho kitaongezeka katika bajeti ijayo ya serikali," alisema Dkt. Kawambwa.

Majibu hayo yaliamsha mori, ambapo wanafunzi walisema hawajaridhika, kwani serikali hivi karibuni ilitaka kuilipa kampuni tata ya Dowans bila kusubiri bajeti ipitishwe bungeni. Pia wakakumbushia wakati wa uchaguzi mwaka jana, serikali ilipoongeza kinyemela mishahara kwa wafanyakazi bila ruksa ya bunge.

Punde mara baada ya Dkt. Kawambwa kuondoka na msafara wake, 'shughuli' ya wanafunzi na askari nayo ikaanza, ambapo vijana wa chuo walianza kurusha chupa za maji na mawe, huku wakijibiwa kwa vishindo vya mabomu ya machozi, hali iliyotifua hali ya hewa na watu kukimbizana hovyo.    

Mpaka Majira linaondoka maeneo hayo, wanafunzi walikuwa wakiendelea kujikusanya, kupeana utaratibu wa kuendeleza mgomo, bila kulazimisha chuo kufungwa, mpaka hapo mwafaka utakapopatikana.

Wakati huo huo, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Elimu cha Mwenge (MWUCE) jana waligoma wakilalalmikia uongozi wa chuo hicho kutokuwa na ushirikiano wanafunzi na kuwaunga mkono wenzao wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Wanafunzi hao katika mgomo huo wafunga geti la chuo hicho ili kuwazuia polisi kuingia ndani ya chuo kwa lengo la kudhibiti mgomo huo kwa madai kuwa wafanyi fujo wala kuharibu mali bali wanadai nyongeza ya posho ya kutoka sh. 5,000 kwa siku kuwa sh. 10,000.

“Rudini kwa kuwa hapa hatufanyi vurugu, hatumdhuru mtu wala mali, tunahitaji fedha zetu hatufungui geti kama mtaingia kwa nguvu mtasababisha vurugu kuzuka,” zilisikika sauti za wanafunzi hao zikiwasihi polisi ambao hata hivyo walitii.

Katika madai yao wanafunzi hao wanasema Bodi ya Mikopo imekuwa ikitoa kiasi cha sh. 500,000 kwa matumizi ya kawaida ya wanachuo, lakini wao wamekuwa wakipewa shs. 470,000 na kwa wale wa mwaka wa pili 300,000 lakini pia wamekuwa wakipewa 270,000 tofauti na vyuo vingine jambo ambalo walihitaji ufafanuzi.

Kwa upande wa fedha za matibabu wanafunzi hao wanadai huchangia sh. 100,000 kwa mwaka lakini kwa matibabu kama upasuaji hutumia fedha zao huku pia asilimia 86 hutumia bima za afya.

Aidha wanafunzi hao wanautuhumu uongozi wa chuo hicho kuendesha chuo kidikteta kwa kuwa wamekuwa hawataki kushughulikia matatizo ya wanafunzi wala majadiliano baina yao.Wanafunzi hao ambao walilinda geti la shule hiyo, hawakutaka mtu yeyote kuingia wala kutoka chuoni hapo isipokuwa waandishi wa habari baada ya kuonesha vitambulisho vyao.

Akizungumza na Majira, Rais wa Serikali ya Wanafunzi hao, Bw. Pontian Kipao alisema wanafunzi hao wamekuwa wakidai fedha za mahitaji maalumu ya vitivo tangu walipoanza mwaka wa kwanza chuoni hapo lakini fedha hizo zimekuwa na mkanganyiko wa nani kati ya wanachuo na uongozi wanaopaswa kuzipangia matumizi.

Bw. Kipao alisema mgomo uliopo chuoni hapo ni halali japo hawajaomba vibali kwa kuwa wanadai mahitaji yao ya msingi ingawa bodi ya mikopo inapaswa kutoa ufafanuzi juu ya fedha hizo.

4 comments:

  1. eng. Mwakapango,E.PAFebruary 8, 2011 at 8:11 AM

    Dr Kawambwa tunajua ulikuwa mlimani pale COET lakini umeshindwa kabisa kutatua kilio cha wanafunzi. mmeongozana na prof. Dihenga ambaye pia alikuwa chuo kikuu cha Sokoine ambaye naye amekuwa chanzo kikubwa cha matatizo hayo. kwa kumbukumbu yangu allowance ya sh.5000/= ilianza kutolewa mwaka 2006 au 2005 sasa najiuliza ni creteria gani wanatumia kutengeza hiyo posho za wanafunzi mfano chai shilingi ngapi? chakula cha mchana shilingi ngapi? chakula cha jioni shilingi ngapi? fedha ya malazi shilingi ngapi? na matumizi mengineyo ni shilingi ngapi? toka miaka hiyo shilingi elfu tano hakuna mabadiliko ya bei? tunatakiwa tusiwafanye dumping place kwa makapi ya chakula ndio wale pamoja na nadhani chakula kibaya kuliko vyote kipo kwenye vyuo vikuu. hivi jamani kina Dr Kawambwa, Prof. Dihenga,na wengineo mnakumbuka mlikuwa mnaimba kuwa mko kilimani mnalanda mnangojea pijo kupanda. wakati huo mafungu yalikuwa yakijitosheleza na mlikula kodi za wananchi mnategemea mtoe wataalamu gani wa kuchukua nafasi zenu? wanasiasa wanatulinganisha na mtoto anayelilia chai wakati hamna majani ya chai wanakaanga sukari ili wsapate rangi ya chai wakati si chai! kama tunashindwa turudishe mfumo wa zamani ambapo serikali iwape chakula bure na shilingi elfu tano ibakie kama subsistsnce. watoto wote wa viongozi wanaosoma kwenye vyuo vya juu wamekuwa wakiishi kwa anasa kuwa magari mazuri ya kifahari na kuishi kwenye majumba ya kifahari yaliyojengwa na babazao kwa kutumia fedha za walalahoi.
    JK Ulipokuwa university ulikuwa makamu wa rsis (DUSO) kilio chako kilikuwa ni kuboresha hali za wanafunzi wapate maisha mazuri ili wawe viongozi bora . hivi mpaka leo wakuletee kilio kile kile nilitegemea utafanya mabaliko makubwa sana bila hata kufuatwa kwa sababu pale mlimani wewe si mgeni ni nyumbani kwako! wasaidieni vijana wa wakulima na wafanyakazi.

    ReplyDelete
  2. Yaani nchi yetu inasikitisha sana, inamaana viongozi hawajui wananchi wanamatatizo gani muhimu wanayotakiwa kutatuliwa hadi waandamane ndo hatua zinachukuliwa, hii ni kazi kubwa, basi kila idara itajiandaa kufanya hivyo maadamu ndo suluhisho la matatizo yao.

    ReplyDelete
  3. je, hao wanafunzi wa Mwenge huwa wanasaini form zenye hayo malipo kutoka wapi? ni Loans board au ni chuo?

    ReplyDelete
  4. Nyie wanafunzi wa UDSM ni kawaida yenu,ikikaribia mitihani ndo mnagoma,experience ya miaka yote inaonesha hivyo,msitubabaishe na madai yenu ya kijinga!!!!! kuna wafanyakazi wanafamilia zao wanaishi kwa hizo hizo hela mnazozigomea,hamna hata haya!!mmejaa ubinafsi tu!

    ReplyDelete