Na Kulwa Mzee, Dodoma
SERIKAlI iko katika hatua za mwisho za kukatisha mkataba na kampuni RITES kwa kuwa imeshindwa kukidhi mategemeo yake ya kulipeleka mbele
zaidi shirika badala ya kurudi nyuma kiutendaji.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Bw. Athumani Mfutakamba alisema hayo jana bungeni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Bariadi Mashariki, Bw. John Cheyo (UDP) aliyetaka kujua serikali ina mpango gani wa kurudisha huduma ya reli ili Watanzania wapate huduma na nchi iendelee.
Bw. Mfutakamba alisema serikali ilikuwa inajaribu kuboresha Shirika la Reli hivyo iliingia ubia ikitegemea shirika kusonga mbele lakini hali haikuwa hivyo.
Alisema sasa serikali inachukua hatua ya kukatisha mkataba na RITES na iko katika hatua za mwisho kukamilisha taratibu za kuvunja mkataba.
"Menejimenti ya RITES walifanya tuwe na safari moja kwa wiki, Desemba mwaka jana tuliongeza safari na kuwa mbili kwa wiki, Juni mwaka huu zitakuwa tatu na Desemba zitakuwa tano," alisema.
Akiuliza swali la msingi kwa niaba ya Mbunge wa Mpanda Mjini, Bw. Said Arfi, Mbunge wa Viti Maalumu 9CHADEMA), Bi. Luhanya Muhonga alitaka kujua lini usafiri wa treni utarudishwa kwenye utaratibu wake wa awali.
Akijibu swali hilo, Bw. Mfutakamba alisema TRL inakabiliwa na upungufu mkubwa wa mapato na vitendea kazi vikiwemo vichwa vya treni na mabehewa, ili kurudisha hali yake serikali imeandaa mpango biashara ambao unahusisha uboreshaji wa miundombinu ya reli na mashine za uendeshaji.
Katika mpango huo alisema sh. bilioni 503.94 zinahitajika katika kipindi cha miaka mitatu ya mwanzo.
No comments:
Post a Comment