09 February 2011

Ilala yapinga kuondolewa kwa mabango

Na Stella Aron

BAADA ya Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kuweka alama za X kwenye mabango mbalimbali katika Mkoa wa Dar es Salaam kwa nia ya
kuondolewa, Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imeibuka na kusema kuwa haitakubaliana na uamuzi huo kwa madai umefanywa kwa kukurupuka.

Manispaa hiyo imesema kuwa imesikitishwa na kitendo cha TANROADS ambacho hakikufuata sheria jambo ambalo linaweza kuisababishia manispaa hiyo na nyingine kuingia kwenye kesi.

Hatua hiyo imetolewa kwenye kikao cha Kamati ya Mapato na Matumizi cha halmashauri hiyo kilichofanyika jana katika ukumbi wa wa manispaa hiyo wa Arnatouglu.

Akizungumza kwenye kikao hicho Meya wa manispaa hiyo, Bw. Jerry Slaa ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati hiyo alisema manispaa hiyi tayari imeweka ulinzi kuhakikisha kuwa kuwa mabango hayo hayaondolewi.

"Tangu wiki iliyopita tumeanza ulinzi ili kuhakikisha kuwa mabango hayo hayabomolewi kwa kuwa TANROADS hawakutushirikisha katika maamuzi yao na tukisema tuache basi sisi tutapelekwa mahakamani kwa ajili ya kulipa fidia na pesa mabango hayo ambazo hatuna," alisema Bw. Jerry.

Alisema kuwa manispaa hiyo ilikuwa ikipata fedha zaidi ya sh. bilioni 2 ambazo zilikuwa zikisaidia katika ujenzi na ukarabati wa barabara za ndani, usafi, ujenzi wa mitaro, ukataji wa nyasi na mengine mengi.

Amesema kuwa TANROADS haikuwashirikisha wadau ambao ndio wanaolengwa kutokana kuruhusu ujenzi na ubomolewa na mabngo ndani katika manispaa.

Alisema kuwa endapo mabango hayo yatabomolewa kuna uwezekano mkubwa wa wafanyabiashara kwenda mahakamani kudai malipo yao pamoja na fidia kutokana na manispaa hiyo kutoa kibali kwa ajili ya uwekaji wa mabango hayo.

Alisema kuwa kutokana na kuwekwa kwa alama hizo jiji limeonekana kuwa chafu na hata baadhi ya wananchi na wafanyabiashara wameingia na hofu licha ya watalii wengine kudhani kuwa ni nembo ya jiji.

Alisema kabla ya kuwekwa kwa alama hizo TANROADS ilitakiwa kushirikiana na manispaa hiyo na kuangalia uwezekano wa kuwaandikia barua wahusika na namna za kulitatua na si kukurupuka kama ilivyofanya.

Kutokana na kero hiyo manispaa hiyo imeazimia kwenda kumwona Waziri Mkuu Bw. Mizengo Pinda ili kuweza kulitafutia ufumbuzi wa haraka suala hilo.

No comments:

Post a Comment