24 February 2011

Mgawo sasa swali gumu

*TANESCO, wabunge wakosa majawabu
*Wagonganisha vichwa nini kifanywe


Na Tumaini Makene

HATMA ya mgawo wa umeme unaoendelea nchini kwa takribani miezi mitatu sasa bado ni kizungumkuti, huku
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ikikutana na watendaji wa Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (TANESCO) kwa saa tano bila suluhisho mwafaka.

Wakati kamati hiyo pamoja na watendaji wa TANESCO wakizungumzia kuwasha mitambo ya kampuni tata ya Dowans kama moja ya njia ya dharura ya kupunguza ama kumaliza tatizo la mgawo wa umeme, Majira limeelezwa kuwa iwapo hatua hiyo itafanyika bila ruksa ya bunge, itakuwa na sawa na kudharau mhimili huo wa dola, kutokana na azimio lake miaka mitatu iliyopita.

Mmoja wa wabunge wa Kamati ya Nishati na Madini, ambaye alizungumza na Majira katika hali ya kutoandikwa jina lake gazetini, alisema kuwa mbali ya kuweza kulidharau bunge, kuwasha mitambo ya Dowans kama moja ya suluhisho, ina lengo la kutaka kuisafisha kampuni hiyo ionekane kuwa haina tatizo, hivyo kuondoa utata wake uliosababisha mkataba wake na TANESCO wa kuzalisha umeme, ukavunjwa mwaka 2008.

Wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini, chini ya uenyekiti wa Mbunge wa Bumbuli (CCM), Bw. January Makamba jana kabla ya kukutana na watendaji wa TANESCO, ilikuwa na kikao kifupi kilichoonekana kuwa ni cha maandalizi katika ofisi ndogo za Bunge Dar es Salaam, kabla ya kuanza safari kwenda makao makuu ya shirika hilo.

Wakiwa makao makuu ya shirika hilo, ndani ya kikao baada ya kuwaomba waandishi wa habari wapishe, wajumbe wa kamati na watendaji wa TANESCO walitumia takribani saa tano, kuanzia saa tano asubuhi mpaka saa 10 jioni kupata mapumziko ya muda mfupi kwa chakula cha mchana, huku mambo yakionekana kuwa moto.

Mara kadhaa, watendaji wa TANESCO na wabunge walikuwa wakitengana kwa muda kisha kukutana tena, hali ambayo ilielezewa baadaye na Bw. Makamba kuwa wakati mwingine ililazimika kamati hiyo kuendesha vikao vyake kwa mujibu wa kanuni na taratibu za kibunge na watendaji nao kwenda kujadili pembeni masuala yaliyoibuka katika kikao, kisha pande mbili hizo kukutana tena kuendeleza mjadala kikaoni.

"Ndani tumepokea na kujadili taarifa ya watendaji wa TANESCO ambayo kwa kweli ukiachilia mbali usahihi, ina mambo mengi ikielezea kwa kina sana, wametoa taarifa yao juu ya hali ya mgawo wa umeme, nasi tumeuliza maswali na kutoa ushauri namna gani hatua za kusaidia ziwe za haraka zaidi, kwa sababu TANESCO ina biashara ya kuwasha umeme si kuzuia umeme.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari juu ya mipango ya dharura ya kupunguza au kumaliza mgawo wa umeme, iliyojadiliwa katika kikao hicho Bw. Makamba alisema;

"Ndiyo suala la kuwasha mitambo ya Dowans imejadiliwa ikiwa ni moja ya hatua ya dharura, na wenye mitambo walikuwa hapa nchini na walizungumza na TANESCO, lakini imeshauriwa kuwa suala hilo liangaliwe vizuri, lizungumzwe bila kuathiri kesi iliyoko mahakamani...maana suala hili lina mambo mengi ndani yake;

"Kuna masuala ya kisheria, kisiasa na kiuchumi...mipango mingine iliyojadiliwa ni kuhusu ununuzi wa majenereta ya diseli ambayo yanaweza kuzalisha megawati 260, ambayo yanaweza kupatikana mwezi Juni au Julai. Pia kuna mpango wa kuzalisha megawati 100 kwa gesi hapa Dar es Salaam na megawati 60 kwa mafuta huko Mwanza," alisema Bw. Makamba kabla ya kuendelea na kikao baada ya mapumziko.

Mapema wakati akifungua kikao cha jana, Bw. Makamba alisema kuwa mbali ya kutambuana, kutaka kujua namna shirika hilo linavyoendeshwa, hali ya uzalishaji wa umeme nchini, suala la muhimu ambalo wajumbe wa kikao walipaswa kujikita kujadili ni 'kwa taarifa sahihi, za ukweli na uwazi, namna gani na lini mgawo wa umeme utamalizika nchini'.

Lakini akizungumza na waandishi wa habari, Bw. Makamba alisema kuwa mpaka wanafikia mapumziko, baada ya kuwa wamesikiliza taarifa hiyo aliyoita ya kina kutoka TANESCO na kujadiliana kwa saa tano, kikao hicho kilikuwa bado hakijafikia suluhisho mwafaka hasa juu ya namna gani na lini, mgawo wa umeme unaoendelea kuathiri uchumi na maisha ya kila siku ya Watanzania, utamalizika.

Mpaka Majira linaondoka eneo la kikao, makao makuu ya TANESCO, wajumbe walikuwa wakiendelea na mjadala, ambao mmoja wa maofisa wa bunge wanaohusika katika kamati hiyo ilithibitisha kuwa 'kikao kilikuwa moto kweli'.

5 comments:

  1. Hivi huu mgao mpaka lini jamani!kila siku mgao mgao tuu kana kwamba nchi haina vyanzo vya kuondoa tatizo hili!mi naona shida sio vyanzo shida ni watu hapa.uwezo wao ni mdogo wa kuona mbali na kuweza kuondoa haya matatizo,hebu leo fikiria tuna vyanzo vingapi vya kuweza kuzalisha umeme......!ni vingi tu havina idadi.leo mungu ametupa gas pia tuna mto rufiji hivi bado mpaka leo tunajadili suala la umeme tu! ni aibu hii na hii inaonyesha kwamba sisi hatuna mipango,sijui kizazi chetu kinachokuja wataishi vipi katika hali hii!nashauri ikiwa leo dowans wanadai fidia ya mabilion basi hizo fedha bora zianze kuingizwa katika kuandaa mpango wa kuzalisha umeme kutoka mto rufiji ambao kama serikali itaupa kipau mbele hii shida yote itaondoka na kuwa historia.kusini Mungu ameipa utajiri wa raslimali nyingi tu ikiwemo gas kama sikosei inaanzia hapo mkuranga,kilwa mpanga mtwara kwa nini tusijipange kwa haya ukichanganya na mto rufiji naimani tutakuwa hatuna shida tena na hili la umeme.MUNGU wape roho za imani viongozi wetu wajue tunajenga nchi yetu ambao wao wakifa watazikwa hapa hapa.

    ReplyDelete
  2. Jamani kwa Tanzania Majenerator hayataweza kuondoa tatizo la umeme, Vyanzo vyote vya umeme vilivyotajwa hapo juu havitufikishi mbali. Nategemea tufikirie umeme wa maji, Tanzania Tanzania tunamito mingi Mikubwa, Pia umeme wa Makaa ya mawe, tunamigodi ya makaa ya mawe mingi mikubwa. Hili swala la Majerata, linawasaidia watu kuchakachua tu wala halitaondoa tatizo la umeme.

    ReplyDelete
  3. Nadhani mgawo wa umeme utaisha pale tutakapoacha kuchanganya siasa na taaluma. Mkataba wa mwanzo wa Tanesco na Dowans haukuwa na tatizo. Jeuri ya kisiasa na kujaa maji kwenye mabwawa wakati ule ndio kulitufanya tuone Dowans haina maana. Kwa sasa tumekwama lakini bado tunaona tukiwasha mitambo bunge litadhalilika! Basi tuombe Mungu ashushe mvua!

    ReplyDelete
  4. Kwa kweli nimechoka kusikia ufisadi, Downans, & richmond kila siku kwenye habari za umeme. Halafu tukiambiwa Watanzania tuna akili finyu tunakasirika. Je Mahakama ya kitaifa pia ni mafisadi? ikiwa wameweza kuona kuwa Tanesco wamefanya makosa vipi wananchi pia tusione kuwa uamuzi wa kusimamisha mikataba ili kupata sifa kisiasa ni mbovu?
    Watanzania hatuna upewo wa kuchambua mambo badala yake tunakubali kuendeshwa na wanasiasa. ATCL pia imeshindwa mahakama, je ni ufisadi? mbona hatuoni habari kila siku kuhusu kesi hiyo?
    Umeme ni tatizo na umetokana na nchi kutokuwa na dira. IPTL inazalisha 10MW mchana na 50MW usiku kwa sababu Tanesco haina fedha, fedha zote zimeenda wapi? Mbona wakati wa uchaguzi fedha zilikuweko?
    Naomba watanzania tuamke na kutumia juhudi zetu kuuliza serekali na tanesco wanatupeleka wapi.
    Tanesco hawatengenezi umeme mpaka wapewe rushwa, huo sio ufisadi? Tusitofautishe hongo ndogo na kubwa kwani hatutatenda haki kwa jamii.
    Tanzania bila rushwa inawezekana

    ReplyDelete
  5. mwenyezi mungu atusaidie,inabidi tuanze kuliombea taifa letu Mungu ndiiye atakaye tuondoa katika matatizo haya.

    ReplyDelete