08 February 2011

'Katiba isiharakishwe kama zimamoto'

Na Grace Michael

ASASI za Kiraia zilizoungana na kuunda Jukwaa la Katiba Tanzania limesema kuwa hakuna sababu yoyote ya kukimbiza mchakato wa uandikwaji wa
katiba mpya kama zima moto kwa kuwa  unatakiwa kufuata ngazi za kitaalamu huku ukiwahusisha wananchi wote ambao ndio wenye katiba.

Mbali na hiyo jukwaa hilo limetoa mwito kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuandaa na kupeleka haraka muswada bungeni ambao utatoa mwongozo au taratubu za kufuatwa katika uandikwaji wa katiba mpya ambao utazingatia hatua sita za kitaalamu ili kukidhi mahitaji yaliyopo kwa sasa.

“Tusiwe na haraka ya zima moto katika uandikaji wa katiba, bali twende hatua kwa hatua, na mchakato usitekwe na chama chochote cha kisiasa kwa kuwa katiba ni mali ya wananchi.


"Kinachotakiwa ni kuhakikisha wananchi wanashirikishwa katika hatua zote ili hatimaye waamue nini kiwemo na nini kisiwemo katika katiba mpya,” alisema Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Bw. Deus Kibamba.

Alisema kuwa wao kama jukwaa la Katiba Tanzania wana jukumu kubwa la kuwezesha uelewa na ushiriki wa wananchi katika mchakato wa kuandaa katiba mpya, hivyo watahamasisha wananchi ili waweze kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuandaa katiba mpya.

Alizitaja taratibu ambazo wangependa zifuatwe katika mchakato huo kuwa ni pamoja na kuwepo kwa mijadala ya awali ya wananchi ambayo itawawezesha kuibua, kujadili na kukubaliana mambo yanayotakiwa kuzingatiwa katika kuandika katiba hiyo.

Hatua ya pili alisema kuwepo kwa mkutano mkuu wa kitaifa wa katiba kwa ajili ya kuchambua mambo yaliyoibuliwa na wananchi na kupangwa katika makundi yanayoweza kujadilika kimafungu na baada ya hapo iwepo tume ya wataalamu ya katiba ambayo itaratibu maoni ya wananchi na kuyaweka katika waraka maalumu na tume hii itapaswa kuwajibika bungeni na jukwaa litashiriki kufuatilia uundwaji na ufanisi wa utendaji wake.

Bw. Kibamba aliendelea kueleza kuwa hatua inayotakiwa kufuatwa ni kuandaliwa kwa rasimu ya katiba na kuwasilishwa mbele ya bunge maalumu la katiba ambalo litaundwa kwa utaratibu maalumu ambalo litakuwa tofauti na bunge la kawaida na litashirikisha wawakilishi kutoka makundi ya kijamii mijini na vijijini Tanzania Bara na Visiwani.

Hatua ya mwisho ni kura ya maoni ya katiba ambayo itapigwa nchi nzima na wananchi wote wenye sifa ya kupiga kura na jukwaa litahamasisha wapiga kura kushiriki kikamilifu katika kura ya maamuzi na vigezo vya kura hiyo vitazingatiwa.

Kutokana na hayo, jukwaa hilo lilisisitiza kila mmoja kwa nafasi yake kuhakikisha anashiriki kikamilifu katika mchakato huo ili suala hilo liweze kufanikiwa na hatimaye kuondokana na matatizo yanayosababishwa na mapungufu ya katiba ya sasa.

Akizungumzia baadhi ya mapungufu ya katiba ya sasa alisema kuwa haitoi mwelekeo wa maendeleo ya nchi, inatumika zaidi kama nyenzo ya dola kudhibiti wananchi kujiletea maendeleo, haibainishi makubaliano ya kisiasa baina ya wananchi na viongozi wa dola lakini pia inamilikisha mamlaka makubwa kupita kiasi kwa rais badala ya kutoa mgawanyo sawa wa mamlaka kwa mihimi mitatu ya dola.

Asasi hizo ni pamoja na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Chama cha waandishi wa habari wanawake, SAHRINGON, Haki Ardhi, TCIB, TCDD, TANLAP, TANEPHA, EHE, TANGO, YPC na TLF.

6 comments:

  1. Ama kweli akili mali.. sasa wenzetu mliojichukulia jukwaa na kusema mna "umhimu mkubwa" nani kawapa jukumu hilo?

    Haya, mnasema "Bunge Maalum" linatoka wapi tofauti na lile lililochaguliwa na wananchi kidemocrasia? Jamani, hatuwezi kutafuta democrasia kwa kuvunja democrasia!! Ondoeni nadharia, na tukabiliane na hali halisi. Tuelewesheni kwanza - je hayo mabadiliko ya katiba, kwa mujibu wa uchambuzi wenu wana jukwaa yanahusisha asilimia ngapi ya KATIBA yetu? Tuanzie hapo...

    ReplyDelete
  2. Kwenye katiba mpya iwekwe wazi kuwa tututaki wakuu wa mikoa na wilaya.Hakuna haja ya wakuu hao. Mfano mkuu wa wilaya ya morogoro anishi mjini wala watu hawamjui naye hana habari ya kasanga wala kisagira anazisikia kwenye bomba tu.
    Please remove them. tunataka meya na council na wakuu wa kata, hata tarafa hatuwahitaji. iwe meya,baraza la jiji au mji (12 kila mmoja department yake)na mkuu wa kata na kijiji basi tutasonga mbele. Mstari wa uongozi ni mkubwa mno. Mkoa unahitaji meya mmoja tu na wasaidizi 12 hao wagawiwe wizara.

    ReplyDelete
  3. Katiba tunaitaka. Tunaitaka lini na kwa namna gani ni jukumu la wananchi na kwa kupitia wawakilishi wetu.

    Watu wasitulazimishe kukubali ushauri wao! Hapa tulipofikia ni kama tunatazamana na ajali. Hatuhitaji kusubiri. Tunahitaji katiba.

    Hii sio enzi ya ujima ambapo ilikuwa inachukua muda wa miaka mpaka taarifa ziwafikie wananchi. Hii ni ENZI YA TEKNOHAMA, toa sema kitu leo, kesho utakuta kinaongelewa kijijini. Ukitangaza leo kesho wakatoe maoni yao kuhusu katiba haitachukua muda wooote watapanga foleni.

    Serikali toeni utaratibu wa kuandika, kama hamna hela za kutoa elimu kwa jamii, sisi tutawapigia simu ndugu zetu wa vijijini, wala msipate shida. Mradi tu muwapeleke watu wa kukusanya maoni.

    Hizi za kutuambia katiba isiharakishwe ni za enzi zilizopitwa. Kwa nini mpaka muone watu wanakufa ndio mjue kuna hatari.

    Heri kinga kuliko tiba!!

    ReplyDelete
  4. Hakuna haraka,wala hatutaki watu wajipatie umaarufu kwa hili,watu walitaka katiba mpya siku nyingi tu na hawa waliojitokeza sasa ni baada ya kuona maslahi yao ya kisiasa yanakwama kutokana na katiba mpya ndio wamekuja na mbinu mpya ya kuidai,ni ujinga kutegemea wawakilishi wetu bungeni ndio watutengezee katiba mpya,hawa hujiangalia kwanza wao kisha mwananchi,nani kati ya hao Wabunge kakataa marupurupu na mishahara minono na mafao baada ya miaka mitano kwa kuwa wananchi wananyongwa kwenye mishahara

    ReplyDelete
  5. Tuache ujinga katiba ya zamani watu hawaijui sasa tunataka mpya ili iwe nini? katiba ni ya watu si ya chama fulani. kwanza tunataka watu waijue hii ya sasa ili mpya itapokuja kujadiliwa iwe bora zaidi,yuko mjinga hapo juu ansema ukipuliza baragumu tu kesho watu wako kwenye foleni,hata kama ikiwa kweli mawazo yake ila anajidhihirishia ujinga walio nao Watz,wewe ukapange foleni kitu hujakijua kwa undani kweli?

    ReplyDelete
  6. "kwanza tunataka watu waijue hii ya sasa ili mpya itapokuja kujadiliwa iwe bora zaidi"

    1. "Mnatakwa"! Mlikuwa wapi miaka yote? Shuleni mlikuwa mnatufundisha imani za CCM, leo mnataka watu waijue katiba!

    2. Mtaanza lini?

    ReplyDelete