11 February 2011

Hotuba ya JK bungeni haina jipya-Kafulila

Na Kulwa Mzee, Dodoma

MBUNGE wa Kigoma Kusini, Bw. David Kafulila amesema hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyotoa bungeni Januari mwaka huu haina jipya ni
sawa na aliyotoa mwaka 2009.

Alisema hayo jana bungeni wakati akichangia hotuba ya rais ya kufungua Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 31 mwaka jana, akisema kinachotakiwa kufanyika katika hotuba hiyo ni kusimamia yaliyomo katika hotuba yaingie katika utekelezaji.

Mbunge huyo aliendelea kusema kwamba inasikitisha kwani Watanzania wako katika taifa masikini badala ya kuwahakikishia watawafanyia nini wanatupiana vijembe bungeni.

Alisema ni bahati mbaya hali iliyoko bungeni sasa ni kila mbunge anapigania chama chake badala ya kushirikiana na kufuta tofauti zao.

"Tuna matatizo ya umeme, tunahitaji kuwekeza katika mradi wa umeme, unaenda kutatua mgogoro wa Zimbabwe wakati wa kwako unakushinda," alisema.

Akichangia hotuba hiyo, Mbunge wa Kigoma Kasikazini (CHADEMA), Bw. Zitto Kabwe alisema nchi imekuwa na matabaka ya masikini na tajiri ambapo wenye uwezo wana hospitali zao na usafiri wao.

Alisema hakujawa na sera ya kutengeneza ajira na inawezekanaje kupata ajira wakati hakuna wawekezaji, na mazingira ya uwekezaji yanakuwa mabaya siku hadi siku.

Bw. Zitto alishauri waweke pembeni tofauti zao kwani mwisho wa siku watahojiwa hivyo wajadiliane ni wapi wanalipeleka Taifa kwani hawezi kukubali kuona nchi inasambaratika.

Alisema kila siku waziri anatangaza miradi ya umeme wakati angeweza kuchagua mradi mmoja ili ifike wakati ijulike zimezalishwa megawati ngapi.

Katika hatua nyingine wakati wa kuchangia hotuba hiyo CHADEMA wabunge wa CHADEMA walijikuta wakishambuliwa kwamba wanachambua hotuba ya Rais Kikwete wakati siku alipoitoa walitoka nje na
walisema hawamtambui.

Mashambulizi hayo yalitoka kwa wabunge mbalimbali waliokuwa wakichangia hotuba ya rais katika kipindi cha jioni ambapo walisema watawezaje kuichambua hotuba ambayo hawakuisikiliza.

Akizungumzia hilo Mbunge wa Makete, Bw. Deo Filikunjombe alisema anashangaa kuona wabunge waliotoka nje mara mbili wakisusia bunge leo wanachangia katika hotuba ya rais ambaye hawakumsikiliza.

"Mtu ambaye hujamsikiliza, sijui hotuba hiyo unaitoa wapi na mtu huyo humtambui," alisema.

Alisema anaogopa tabia hiyo anayoiona na endapo viti vingekuwa vinatoka wangefikia hatua ya kurushiana viti ndani ya bunge.

Wakati akisema hayo Mbunge wa Singida Mashariki, Bw. Tindu Lissu aliingilia akisema kwamba kwa mujibu wa kanuni za bunge mbunge haruhusiwi kuzungumza jambo lililo nje ya mjadala.

Hoja hiyo ilijibiwa na Naibu Spika, Bw. Job Ndugay kwa kusema kwamba mbunge yuko ndani ya hoja inayojadiliwa hivyo anaruhusiwa kuendelea kuchangia.

Naibu Spika aliongeza kwamba hakuna kanuni inayomkataza mbunge kuamua kutoka nje, hilo ni jukumu la Watanzania waliompigia kura kumhoji mtu huyo naye atajibu huko.

"Tabia ya kususia bunge na kutoka nje ni ya kuudhi wala haifurahishi hata kidogo," alisema.

Miongoni mwa wabunge wa CHADEMA waliochangia hotuba ya Rais Jakaya Kikwete ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Kabwe, Tindu Lissu na Mbunge wa Mwanza mjini, Bw. Hezekia Wenje.

7 comments:

  1. wabungea kama Filikunjombe ni wa kuonewa huruma kwani wameingia bungeni kwa kashfa kubwa mno. kutoa hongo kubwa hilo pro. mwalyosi maskini huyu anaweza kuthibitisha hilo. aliuza kituo cha mafuta kwa ajili ya kuwahonga wapiga kura katika kula za maoni alikwenda mbali zaidi kwa kuhonga mpaka PCB Hii inasikitisha sana na anasimama kusema kitu ambacho akielewi. Filikunjombe aliwahonga TLP na akamhonga mwanachama wa CHADEMA atoroke na form ili yeye apite bila kupingwa sasa sijui ni mbunge wanani maana yake Ludewa ilikuwa na wapiga kula elfu arobaini yeye alipata kula elfu sita tu. si nia yangu kumzungumzia mtu katika maoni yangu lakini nataka watanzania wajue wanawasikiliza watu wa aina gani bungeni na jinsi gani CCM inazalisha mafisadi.
    hotuba ya rais mimi ambaye siyo mbunge ninayo sembuse kwa mbunge kwani wabunge wote wa CCM walikuwepo siku hiyo? hotuba hiyo imo kwenye makabrasha na imechapishwa na kila mbunge aligawiwa mapema ili aweze kuifuatilia sas hilo bwana Filikunjombe halijui hilo au anadhani hotuba mpaka usikilize hotuba inaweza kusomwa Fililikunjombe inaonekana shule imempiga chenga! Wapiganaji wa CHADEMA nawahakikisha wameisoma na wameiona hamjui kuwa kuna luninga? wao hawakutaka kukaa na JK tu. sasa acheni kupigana vijembe tunataka nondo zishuke?

    ReplyDelete
  2. hivi nyinyi wabunge wetu kweli mnalolote la kujenga taifa hili yaani sijaona fikra zozote.zaidi yakufunga milango tutwangane kwanza,kutoka nje ,amri za kuombana radhi eti mkubwa hadanganyi we makinda usilete heshima za kibena bungeni eti za sikamoo mama,viongozi wakamati wenye kashifa hivi mpaka matapishi yananitoka mtu ameliingiza taifa hili kwenye mateso na madonda bado leo eti bosi wa kamati lo mbumbu chama chetu ssm,pinda unakuelekea si kuzuri tulikuamini sasa unaanza kusema mmmmmmmmmmm,udumu sitta,mwakyembe na shjaa wa ugunduzi na baba wakunusa madhali Dk Slaa.ingaw tumekumisi bungeni.

    ReplyDelete
  3. watu wazima wanajadili hotuba ni pumba tupu hakuna kitu katika hotuba ile inatupotezea mda.

    ReplyDelete
  4. Mi naona ni upuuzi mtu mtupu mtu mzima kusupport ujinga pasipo kufikiri, mimi kwa kweli sijui hii nchi yetu inaelekea wapi hebu watanzania tuamke, tufikiri hasa kauli za viongozi wetu wanazozitoa na pia tuelimike kwani hali ya sasa inatisha sana tumuombe sana Mungu awape hawa viongozi wetu roho ya huruma kwa wananchi wao hasa wale walioko chini ambao hawana kipato vingine tuingie nasi barabarani kama Misri maana tumeshachoshwa.

    ReplyDelete
  5. “CCM limekuwa zimwi tulijualo lakini ambalo linazidi kutula na kutumaliza. HOTUBA GANI HII CHAMAANA HAKUNA. PUMBA TUPU.

    ReplyDelete
  6. Mimi nilitegemea kuwa mwaka huu tuna wabunge vijana wenye uchungu na Taifa letu kumbe ni bora wangebaki walewale. Wewe mbunge nimekuchagua mimi ukaniwakilishe, matokeo yake unaenda kujipendekeza kwa mtu mwingine badala ya kufanya kazi kwa kufuata misingi iliyo bora ili nami nijisifu kuwa kura yangu inalitumikia taifa letu, ninaskitika sana ninapoona mbunge anasifia kitu hata kama anajua fika kuwa ni pumba. Jamani kutenda haki kwa wananchi wenu waliowapelekeni bungeni 2015 sio mbali.

    ReplyDelete
  7. Kwa binadamu mstaarabu na mcha MUNGU kuendekeza mvutano usiomletea tija mwananchi mnyonge aliyekubali kuacha kupika maandazi na kuwahi kujipanga mstarini kukuchagua wewe kumwakilisha Mjengoni ni kumnyonya.Hujisikii vibaya kupokea posho iliyonona itokanayo na kodi ya wakulima na wafanyakazi maskini wa kutupwa kwa kususia vikao na kuendekeza malumbano ya ki-itikadi badala ya kujadili njia zinazopaswa kufuatwa na Serikali ili angalau kupunguza kama si kuondoa kabisa makali ya umaskini kwa Watanzania walio wengi? Kuna faida gani ya wewe kuwa Mbunge? Dhambi ya UROHO na UBINAFSI HAISAMEHEKI mbele ya Mwenyezi Mungu-ACHA Kuitumikia nafsi yako pekee.

    ReplyDelete