Na Rabia Bakari
KAMPUNI ya Mawakili ya Rex iliyoiwakilisha TANESCO katika kesi dhidi ya Dowans imetajwa mbele ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kuwa
ilihusika katika kesi hiyo ikiwa na mgongano wa kimaslahi.
Hayo yalifahamika jana baada ya kamati hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Bw. Januari Makamba ilipotembelea mitambo ya Dowans, na katika maelezo ya mmoja wa wanahisa na Mkurugenzi wa Fedha wa Dowans Tanzania Limited, Bw. Stanley Munai ilibainika kuwa kampuni ya REX ilikuwa inatoa msaada wa kisheria kwa pande mbili katika kesi hiyo.
Maelezo hayo yalijitokezo wakati Bw. Munai akijibu maswali kuhusu madeni yanayikali kampuni hiyo ambayo imekuwa gumzo la muda mrefu hapa nchini.
Bw. Munai alisema kuhusu madeni hawana cha kuficha, kwamba wanadaiwa dola milioni mbili na benki ya Barclays, na kabla ya deni hilo na benki hiyo, walikuwa wamechukua mkopo katika benki ya Stanbic wa dola milioni 20 ambako walihamishia deni hilo Barclays kutokana na makato ya Stanbic kuwa makubwa.
Alisema wakati wa kuchukua mkopo Stanbic, benki hiyo iliwaonesha orodha ya kampuni za mawakili na kuwataka kuchagua mojawapo kwa ajili ya kuwakagua na kuwathibitisha ili waweze kupata mkopo ambapo walichagua Kampuni ya Mawakili ya REX, ambayo iliwaandikia maoni 'mazuri' na kuwathitisha wapate mkopo huo.
Kauli hiyo ilisababisha baadhi ya wabunge wahoji, iweje mawakili hao wa REX wawathibitishe Dowans kupata mkopo, wakati huo huo ndio walikuwa wawakilishi wa wapinzani wao TANESCO katika kesi iliyokuwa ikisikilizwa ICC.
Akijibu hilo, Bw. Munai alidai kuwa hofu hiyo hata wao aliiona mapema na kwa ushauri waliwaandikia barua TANESCO kuwajulisha kuwa mawakili hao wana mgongano wa kimaslahi na kuwa haitakuwa vizuri kuwawakilisha TANESCO, lakini hawakuji na matokeo yake mawakili waliendelea kusimamia kesi hiyo, huku akidai kuwa hawakujua kwa nini TANESCO waliamua kukaa kimya.
Kauli hiyo iliwafanya wabunge wengi kutingisha kishwa na kumwambia mkurugenzi huyo kuwa wameshaelewa, na hilo si la kwake yeye.
Akiendelea kubanwa na maswali ya papo hapo kwa hapo ya wabunge hao, ambapo kwa kiasi kikubwa Bw. Makamba ndio alikuwa akiuliza maswali mfululizo, pia alitaka kufahamu sababu kubwa iliyofanya mmiliki wa Dowans, Sulaiman Mohamed Yahya Al Adawi kuja nchini na kutaka kuzungumza na TANESCO.
"Alikuja nchini (Al Adawi) baada ya kusikia malalamiko ya Watanzania kuwa fedha tunazodai ni nyingi, na lengo likiwa ni kuzungumza na TANESCO ili kukubaliana gharama za kupunguza na hatimaye kama inawezekana tuendelee kutoa huduma, lakini hata hivyo TNAESCO hawajajibu barua hiyo ya kutaka tuonane nao na wala hawataki kukaa pamoja nasi," aliongeza Bw. Munai.
Alisema kuwa Bw. Al Adawi alikuwa tayari kupata hasara na kusamehe mambo mengi, lakini TANESCO hawaoneshi ushirikiano katika hilo.
Bw. Mkamba alitaka kujua hasara gani ambayo Bw. Al Adawi yupo tayari
kuipata na kuwasaidia Watanzania, na Bw. Munai alijibu kuwa "Yeye
amewekeza mitambo yake ipo hapa, na inawashwa ili isioze, kuna umeme tunatumia, bima ya tahadhari inalipwa, tunalipa watu wanaokuja kufanya kazi, ni gharama kubwa tunatumia, lakini yupo tayari kupata hasara kwa hilo."
Baada ya wanakamati kuondoka waandishi walimganda Bw. Munai kutaka kujua mambo kadhaa ikiwemo uhalali wa deni na gharama halisi wanazodai kwa TANESCO, ambapo alijibu kuwa ni nyingi mno, kwani hata hizo bilioni 94 zinazosemwa ni nyuma kabla ya hukumu kutoka, ambapo kwa makubaliano TANESCO walitakiwa kuwalipa dola 11,800 kila siku na fedha hizo zilianza kuhesabika kuanzia Juni 14, mwaka jana hadi leo.
Katika hatua nyingine, Dowans imeitupia lawama TANESCO kuwa ndio chanzo cha matatizo baada ya kutotaka kujibu barua mbalimbali walizoandikiwa wala kutotaka kukaa mezani kwa ajili ya kushauriana kuwapa 'unafuu' Watanzania.
Awali, baada ya kamati hiyo kuingia katika eneo la mitambo ya Dowans, Mkurugenzi wa Uzalishaji wa TANESCO, Bw. Moses Mwandenga alianza kutoa maelezo ya mitambo hiyo jinsi inavyowashwa na kufanya kazi, ambapo alielezea uwezo wa kuzalisha umeme na jinsi unavyoingia katika gridi ya taifa.
Mtaalamu huyo alieleza kuwa tangu mkataba wao na TANESCO uvunjwe, ili
kudhibiti uharibifu wa vifaa mitambo hiyo huwashwa na kila baada ya wiki mbili ili kuhakikisha inafanya kazi lakini bila kuzalisha umeme.
Baadhi ya wanakamati walitaka kujua hali ya mitambo wakati inaingizwa nchini ambapo, Bw. Munai alijibu kuwa ilikuwa mipya, na kuonesha kuchukizwa na kauli za baadhi ya watu wanaodai kuwa mitambo hiyo ni chakavu.
Alisema mitambo yote iliingia nchini ikiwa mipya isipokuwa mmoja, uliokuwa umetumika kwa saa 5,000, muda ambao alidai ni mfupi kwa kifaa kipya.
Baada ya maswali ya kitaalamu ndipo, Bw. Makamba alimpotaka mkurugenzi huyo kueleza ni kwanini hawataki kuondoa mitambo yao ilihali haifanyi kazi yoyote na kung'ang'ania kubaki nchini.
"Hatujang'ang'ania, isipokuwa baada ya TANESCO kuvunja mtakaba, tulitaka kuondoa mitambo, wao wakatuzuia kuwa mpaka kesi iliyopo ICC itakapomalizika ndipo tunaweza kuondoka," alisema Bw. Munai.
Aliendelea kujitetea kuwa kesi hiyo imeisha muda si mrefu, lakini ni mapema mno kwao kueleza hatua za kuondoka kwa sasa.
Baada ya ziara, waandishi walimgeukia Bw. Makamba kutaka maoni yake, ambapo alikiri kuona matatizo mengi, na kudai kuwa hawezi kuongea hapo isipokuwa leo ambapo kamati itakutana na wadau wote wanaozalisha umeme.
"Nadhani ndugu waandishi na nyie mmejionea kila kitu, sasa mimi sina cha kusema kwa leo, isipokuwa kesho tutazungumza baada ya kukutana na wadu wote wakiwemo Songas, Dowans, TANESCO na wengineo," alijibu.
ukweli utajulikana tuu. mambo yanaanza kidogo kidogo kufunguka. waandishi tunawaomba wasilalie upande mmoja endeleeni kutupa ukweli kadri unavyojitokeza. maana tumedanganywa sana mpaka kufika mahala wananchi kiuona Dowans kama vile adui mkubwa wa watanzania. kumbe kikulacho kinguoni mwako. huu ni wakati wa watanzania kuzipa akili zetu nafasi badala ya kukurupuka na kujaa jazba zenye maslahi ya kisiasa ya baadhi ya watu. Mh. Makamba endelea na shughuli za kamati yako, nadhani sasa tumeanza kuona ukweli wa jambo hili. unaelekea kuzuri. ukweli utajulikana tuu. kama kosa ni la Dowans,Tanesco au bunge lililopita?
ReplyDeleteUkweli ni kwamba viongozi wa ngazi ya juu ya serikali ya CCM ilihusika na uchafu huu wa Dowans na zipo dalili tosha kwamba ufisadi huu ulisaidia katika uchaguzi wa mwaka 2006 wakati Rostam Aziz akiwa mweka hazina wa CCM. Sio tu Dowans bali pia EPA, Twin Towers, na mauchafu mengine. Mkiambiwa CCM imeoza na inanuka mnakana. Siku moja yatawatokea puani.
ReplyDeleteHii yote, ni gia ya kuipigia upatu Dowans, ipate kazi nyingine ya kuzalisha umeme! Baadae mtasikia, mitambo yao inanunuliwa na Tanesco! Ukweli ni kuwa, Dowans hawana pa kupeleka hiyo mitambo, wala hawana sehemu nyingine wanapofanya kazi au wanapoweza kupata kazi ya kufua na kulangua umeme, zaidi ya Tanzania. Huyu Makamba ni dalali tu!
ReplyDeletePiga ua galagaza hii ni mbinu iliyo ndani ya Serikali yetu, na wote kuanzia Raisi wetu anaujua kwa undani UCHAFU huu kinachofanyika sasa ni kiini macho tu.
ReplyDeleteNakumbuka niliwahi kusoma katika gazeti la Mwana halisi kuhusu utata wa wanasheria wa kampuni ya REX kutetea/kuhusika katika maswala ya kisheria kati ya TANESCO na DOWANS, kitu ambacho ni cha ajabu mno.(maslahi GONGANA)
Aliyekwambia vunja mkataba ndiye anakuwa mwakilishi wako na wa ulivunja mkataba naye hapa lazima kuna namna, tumefanywa wajinga kwelikweli, hatunazo, TUMEFULIA, wala hatuoni kama tu UCHI. (pamoja na vyuo vikuu kibao!! Maprofesa kibao !!! na Udaktari waKO wa heshima !!!) Vimeshindwa kukabiliana na UCHAFU HUU.
Asante RAISI wetu JAKAYA MRISHO KIKWETE kwa kutufikisha hapa, maana tulipofika mhh ni mahali PAZURI panatia matumaini ya MAISHA BORA KWA KILA MTANZANIA huku tukiwa GIZANI!!!!!
Viongozi wa Tanesco hawataki kukutana na Dowans kwa kuogopa kuumbuka, watuele waliwezaje kutumia kampuni ya uwakili ya Rex wakati wametaarifiwa kwamba kampuni hiyo tayari inaiwakilisha Dowans? Nadhani hapa kuna mchezo wameucheza, lakini pamoja na hayo bado tatizo la umeme liko palepale tunahitaji ufumbuzi wa haraka. Tanesco hawataki kukutana na Dowans ili matatizo ya umeme yawe makubwa zaidi ili wapate dili la kuagiza mitambo mingine wapate ulaji
ReplyDeleteTumepiga kelele sana juu ya Dowans, lakini kuna haja ya kuangalia na upande mwingine. Siyo vibaya kusema ukweli, kwamba TANESCO wamechemsha sana katika hili. Ukichunguza, kuna kila aina ya uzembe, tena wa makusudi kabisa ambao umefanyika Tanesco, ambao umeendelea kuligharimu taifa hili mabilioni ya shilingi. Uwezekano ni mkubwa kabisa kwamba wapo wanaofaidika na uzembe huu. Ili Serikali iweze kuokoa mabilioni ya mapesa ya Watanzania, ni bora KUIUA TANESCO na kuunda kitu kipya. Hata hapo ilipo tu imekwisha kufa, maana hayo madeni peke yake ya Dowans, ni zaidi ya thamani ya Tanesco yenyewe, sasa si sawasawa na kuifilisi tu?
ReplyDeleteNakubaliana sana na ufumbuzi uliopendekeza Ndugu yangu Ben. Ila utambue kwamba, TANESCO ni kama nembo tu imetumika, wapo wazee wenyewe wanaochezesha mambo huko juu kwa vimemo na kumwambia Mkurugenzi wewe tia saini hapa, au kaseme hiki. Si kweli Tanzania haina rasilimali watu (hata waliopo Tanesco pekeyake) walioshindwa kutatua tatizo la umeme tangu muongo mzima uliopita. Jaribu kuwauliza mainjinia ambao wao hawana nafasi kutokana na siasa kuwameza. Hivyo TANESCO ni pattent ya biashara ya waheshimiwa ambao hawana uchungu wala aibu na Taifa hili. Huwa nasikitika sana ninaposoma maoni ya watu wakisema WASOMO WALIOPO NCHINI HAWANA MSAADA. Ni kweli lazima ionekane hivyo sababu ya mfumo wetu mbovu tunavyoutumia kujiumiza.
ReplyDeleteNakubali kabisa, wanasiasa wanajifanyia maamuzi bila kuwashirikisha wataalamu. Wao wanaangalia faida zao za kisiasa badala ya umma wa Tanzania.
ReplyDeleteKamati ya Makamba inavyohangaika - kutafuta sifa tu! wataalamu wapo na vyombo vya dola vipo, vinafanya nini?
Subiri watakuja na jibu mitambo iwashwe!
Bunge, Mahakama na Serikali (Executive), vyote vipo na vinafanyakazi kuelekea kwenye njia moja ya kuiletea nchi hii/wananchi maendeleo. Na kila chombo kwa namna moja au nyingine kinafanya kazi ya "check-and-balance". itakuwa ni ajabu iwapo Bunge letu litakuwa ni "sehemu ya Serikali" kwa kutofanya kazi zake ipasavyo na "kufunika" "uvundo" unaofanywa na Serikali!!!! Tafadhali sana Wabunge/Kamati za Bunge fanyeni kazi ipasavyo kwani historia itawahukumu!!
ReplyDeleteKumbukeni wapo ambao tayari wamekwishaandika historia zao kwa kulitetea Taifa hili, mfano Dk. Slaa. Huo ni ukweli usiopingika. Sikilizeni Watanzania wanataka nini, hasa kupitia katika vyombo hivi vya habari.
"DOWANS NI CHUI ALIYEJIVIKA NGOZI YA KONDOO"