25 February 2011

Serikali yaweka mikakati kushusha bei ya sukari

Na Tumaini Makene

KUPANDA kwa kasi bei ya sukari kunakoenda sambamba na uhaba wa bidhaa hiyo kwa baadhi ya maeneo nchini kumeishtua serikali na kuamua kuchukua
hatua za haraka zitakazosaidia bidhaa hiyo ishuke na kuuzwa kwa bei elekezi ya sh. 1,700 kwa kilo.

Kumekuwa na taarifa kutoka sehemu mbalimbali nchini, juu ya upatikanaji wa bidhaa hiyo muhimu kwa maisha ya kila siku ya Mtanzania, ikielezwa kuwa bei ya kilo moja sasa imefikia sh. 2,200, mpaka sh. 3,000, huku pia maeneo mengine ya pembezoni yakikumbwa na uhaba.

Akizungumza jana na waandishi wa habari, Waziri wa Viwanda, na Biashara, Dkt. Cyril Chami, alisema kuwa serikali  imebaini tatizo, hali iliyomlazimu Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda kukutana na wadau wote wa sukari nchini ili kutafuta ufumbuzi wa pamoja kuwasaidia wananchi, hususan walaji wa mwisho sokoni.

Kwa mujibu wa Dkt. Chami, katika kikao hicho cha wadau wa sukari na viongozi, ilibainika kuwa hali hiyo (kupanda kwa bei na kukosekana kwa sukari) imetokana na sababu mbili; kupanda kwa bei ya sukari katika soko la dunia na kufungwa kwa viwanda vya sukari nchini (Februari-Mei kila mwaka).

"Katika siku za hivi karibuni, bei ya sukari imekuwa ikipanda kwa kasi katika baadhi ya maeneo nchini na hivyo kuzua hofu kubwa kwa wananchi. Katika maeneo mengine bidhaa hiyo imepungua nkwa kiasi kikubwa jambo linalochangia bei kuzidi kupaa.

"Bei hizo zimekuwa zikiongezeka hadi kufikia wastani wa shilingi 2,200 kwa kilo katika maeneo ya pembezoni mwa nchi. Kutokana na hali hii, Mheshimiwa Waziri Mkuu amekutana na wadau wote wa sukari ili kulipatia tatizo hili ufumbuzi. Wadau hawa ni viongozi wa juu wa wizara na taasisi zinazosimamia uzalishaji na usambazaji wa sukari, wazalishaji wa sukari na wasamabazaji wakuu wa bidhaa hiyo  nchini.

"Katika mkutano huo mambo kadhaa yafuatayo yamebainika; bei ya sukari duniani imepanda sana mwaka huu. Kwa upande wa Tanzania, viwanda hufungwa kati ya miezi ya Februari hadi Mei kila mwaka kwani si msimu wa kuvuna miwa. Wenye viwanda hutumia fursa hiyo kuikarabati mitambo yao wakisubiri msimu wa uzalishaji unaoanza mwzi Juni.

Sababu hizo mbili, kwa mujibu wa Dkt. Chami, zilisababisha wazalishaji na wasambazaji wa bidhaa hiyo, kuhodhi ili bei ikipanda zaidi wanufaike zaidi na pia kwa minajili ya kujilinda dhidi ya washindani wao sokoni, hali iliyoilazimu serikali kufuatilia na kugundua kuwa kiasi cha sukari iliyopo nchini kinatosheleza kwa kwa miezi miwili, bila hata kuhodhiwa.

Kiwango kilichopo cha sukari nchini ambacho kimedaiwa kuhodhiwa kwa makusudi kwa mantiki za kiuchumi ni tani 61,000 wakati mahitaji ya kila mwezi ya sukari nchini ni tani 27,500.

Hivyo ili pengo la mahitaji katika miezi mingine inayobaki (Mei na Juni) kabla ya uzalishaji wa ndani kuanza na kuwa imara tena wakati wa msimu, kiasi cha tani 50,000 kinahitajika kuagizwa kutoka nje ya nchi, hali ambayo imeilazimu serikali kuondoa ushuru kwa sukari itakayoagizwa kutoka nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Hatua ambayo hata hivyo imefikiwa baada ya serikali kuomba kwa jumuiya hiyo na kukubaliwa, kwani kutokana na makubaliano ya Soko la Pamoja la EAC, ni kinyume cha sheria, nchi mwanachama kuagiza bidhaa nje ya jumuiya, bila kutoza kodi.

"Hiyo imekwishazungumziwa tayari, tuliruhusiwa kuagiza hizo tani 50,000 nje ya Afrika Mashariki, lakini tukaona ni vyema tutoe soko kwa sukari ya nchi wanachama wenzetu ambao ni Kenya na Uganda wanaozalisha sukari, hivyo tani 37,500 zitatoka nje ya jumuiya zikiwa zimefutiwa ushuru wa forodha.

'Kiasi kinachobaki cha tani 12,500 kitaagizwa kutoka kwa nchi wanachama hao yaani Kenya na Uganda, ambacho hakihitaji kufutiwa kodi kwani tayari ushuru wake ni sufuri," alisema Dkt. Chami akizungumza na Majira.

Ili kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa ipasavyo, kwa ufanisi na wakati mwafaka, kusaidia usambazaji wa sukari, serikali imeiagiza Mamlaka ya Bandari nchini kuweka kipaumbele kwa meli zitakazoleta sukari, zipakuliwe haraka, kisha Mamlaka ya Mapato (TRA) nayo ichukue hatua kukamilisha taratibu za kutotoza ushuru wa forodha.

Alisema kuwa sukari ya nje, itakayotoka Uganda itasambazwa mikoa ya Kanda ya Ziwa, itakayotoka Kenya itasambazwa mikoa ya Kanda ya Kaskazini, ile ya kutoka Malawi itatumika mikoa ya Kanda ya Kusini na Nyanda za Juu Kusini, huku Dar es Salaam na mikoa mingine ya jirani ikitumia sukari ya Madagascar na Mauritius.

Kwa mpango huo wa kurasimisha uagizaji wa sukari kutoka Malawi kwa ajili ya mikoa ya kusini, itawapatia ahueni wananchi wa maeneo hayo, ambayo nyakati kadhaa, viongozi wao, wakiwemo wabunge walipata kulalamika mbele ya Rais Jakaya Kikwete ugumu wa bidhaa hiyo, kiasi cha kuuzwa sh. 3,000 kwa kilo, kwa maeneo kama vile Tunduma, Mbinga na Kyela.

Aliongeza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wadau katika sekta ndogo ya sukari ili kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa hiyo kwa bei nafuu.

"Ni imani ya serikali kuwa kwa kuwa utekelezaji wa hatua hizi unaanza mara moja, mambo mawili yatatokea. La kwanza, sukari itamfikia kila Mtanzania popote alipo. La pili, bei ya sukari itashuka, na kwa vyovyote vile, pamoja na bei kupanda katika soko la dunia, serikali inategemea kuwa bei itakuwa chini ya shilingi 1,700 kwa kilo hata katika maeneo ya pembezoni kabisa."

Alisema kuwa bei hiyo elekezi imefikiwa na wadau baada ya kukokotoa mahesabu ya gharama zote mpaka hatua ya msambazaji wa mwisho, akiongeza "serikali itafuatilia kwa makini suala hili, haitasita kufunga duka la mtu iwapo atabainika kwenda kinyume baada ya serikali kuwa imeangalia mazingira yote haya kuwasaidia wote, wauzaji na walaji."

"Serikali imeweka utaratibu wa kukutana na wazalishaji na wasambazaji wa sukari mara kwa mara ili kuongeza uzalishaji wa sukari nchini chini ya mpango wa kilimo kwanza na hivyo kuondoa tatizo la upungufu wa sukari nchini," alisema Dkt. Chami akitoa tamko hilo la serikali kuhusu bei ya sukari nchini.

Akifafanua juu ya upandaji wa bidhaa zingine, hususan za chakula katika soko la dunia na nchi maskini kama Tanzania kuathirika pia, alisema zipo sababu kadhaa, ikiwemo kupanda kwa bei ya mafuta ambayo huathiri sekta mbalimbali kwa ujumla na wazalishaji wakubwa duniani wa bidhaa husika kukumbwa na madhira mbalimbali kama majanga ya asili na machafuko. 

No comments:

Post a Comment