15 February 2011

Daladala Mwanza zagoma, abiria wasota

Na Daud Magesa, Mwanza

MADEREVA, makondakta na wapiga debe wa magari madogo yanayosafirisha abiria katikati ya Jiji la Mwanza maarufu kama Express jana waligoma na
ili kuishinikiza serikali kupandisha bei ya nauli.

Mgomo huo ulianza jana saa 3:00 asubuhi na kusababisha usumbufu kwa wakazi wa mkoa huo.

Wakizungumza na Majira nyakati tofauti kuhusu mgomo huo madereva, makondakta na wapiga debe hao walisema wanataka ongezeko la nauli kutoka sh. 250 ya sasa hadi sh. 300 kwa njia fupi na njia ndefu kutoka sh. 450 hadi sh. 500.

Walisema sababu ya kuomba ongezeko hilo ni kutokana na gharama za uendeshaji kupanda ikiwemo ongezeko la bei ya mafuta kutolipwa mishahara na wamiliki wa magari hayo.

Viongozi wa Chama cha Wasafirishaji Mkoa wa Mwanza (MTA), Chama cha Watoa Huduma za Wasafiri (UWATA), Chama cha Madereva Mkoa wa Mwanza (VDA) kwa nyakati tofauti walikiri kuwepo kwa mgomo huo.

Mgomo huo ulisababisha watu mbalimbali kutembea kwa miguu kutoka eneo moja kwenda jingine huku wengine wakipanda pikipiki, bajaj, magari madogo ya mizigo na wale wenye kipato kikubwa kupanda taxi.

Hata hivyo,madereva makondakta waliokataa kushiriki mgomo huo walipigwa mawe na wapiga bede na kufanyiwa fujo kwa kupigwa mawe.

Akizungumza na baada ya kikoa cha Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), Wadau wa Usafiri, wamiliki Vyombo vya Usafiri, Mhandisi wa Jiji, Jeshi la Polisi, Ofisa Mipango MTA, Bw. Robert Mhangwa aliwataka madereva kusitisha mgomo huo na kurejea barabarani.

Alisema iwapo hawatafanya hivyo watachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufutiwa leseni zao.

“Hatuwezi kupandisha nauli kienyeji kwa mgomo bila kufuata taratibu za mamlaka husika, walioitisha mgomo wamekiuka na kuvunja sheria, hivyo wachukuliwe hatua,” aliasema.

Alisema mafuta si chanzo cha athari za vyombo vya usafiri na kusababisha mgomo kwa madereva na kudai tatizo ni vyama vya madereva (VDA) na (MTA) kushindwa kuingia katika ajira rasmi.

“Kutojua sheria si sababu ya kunja sheria, wenzetu madereva ni wagumu kuelewa tulikubaliana waingizwe kwenye ajira , na kila mfanyabiashaa anataka kupata faida.

"Hivyo sheria ipo na lazima iheshimiwe na kuwashutumu trafiki kushindwa kuchukua hatua dhidi ya madereva kwa kusema, mgomo huo si ongezeko la nishati ya mafuta siku zote nyama nono ukimpa masikini itamwozea mkononi,”alisema.

Mwenyekiti wa madereva Bw. Dede Petro alisema kuwa mgomo huo umefanywa na baadhi ya madereva kwa kushirikiana na baadhi ya wamiliki wa magari na wapiga debe

Afisa Mfawidhi wa SUMATRA Kanda ya Ziwa Bw.Alfred Waryana alilaani mgomo huo na kusema ni batili na kuwataka wamiliki kuzingatia makubaliano ya kikao cha wadau cha Januari 10 mwaka huu ambacho kiliwataka watoe mchanganuo wa maombi yao ya kupandisha nauli.

“Katika kikao hicho wadau wote tulihusika tukawaomba mtoe mchanganuo wa ombi lenu la kupandisha nauli, lakini hadi leo hamjatoa mchanganuo mnagoma, Mamlaka huwa inapitia maudhui ya wadau wote kwanza kabla ya kufukia uamuzi wa upandisha viwango vya nauli, hivyo leteni nyaraka (document) hiyo kwanza tuione kwanini mnaomba nauli ipande.” alisema Bw.Waryana.

Kikao hicho ambacho kilikuwa chini ya Mwenyekiti Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Simon Sirro, kiliwaagiza viongozi wa madereva na chama cha wasafirishaji Mwanza kupitia kwa kiongozi wao Bw. Julius Maresi, warejeshe huduma kabla ya saa 9 mchana ili wananchi wasiendelee kupata tabu ya usafiri.

Kamanda Sirro akifunga kikao hicho alisema kwamba, kuanzia mchana jana polisi, waliingia mitaani kukabiliana na wapigadebe na makondakta watakaozuia magari yasitoe huduma kama walivyokuwa wakiyazuia asubuhi na kwamba magari yatakayoendelea kugoma yatachukuliwa hatua.

Mdau mwingine ambaye hakutaka jina kutajwa gazetini alihoji ni vipi madereva na makondakta wawe na nguvu kuliko wamiliki wa magari kiasi cha kuyaondoa magari hayo barabarani na kushindwa kusafirisha abiria kwa vile wanafanya kazi kwa mikataba.

Hadi tukienda majia ya saa 10:30 hakuna daladala zilizokuwa zimeanza kutoa huduma huku wananchi wakiendelea kutembea kwa miguu na wenmgine wakitumia usafiri wa pikipiki kwa gharama ya sh. 1000.

1 comment: