25 February 2011

Adaiwa kubomoa nyumba alipwe fidia

Na Peter Mwenda

MKAZI mmoja wa Kinyerezi amedaiwa kubomoa nyumba yake ili ionekane imebomolewa na milipuko ya mabomu na hatimaye alipwe fidia.Kaimu Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Saidi Meki Sadiki akizungumza na waandishi wa habari jana alisema mkazi huyo alifika kuwataka aorodheshwe kuwa ameathirika na mabomu wakati si kweli.

Alisema hiyo moja ya matukio ambayo yanawafikia Kamati ya maafa kwani kuna baadhi ya watu wasio waaminifu wanatumia nafasi hiyo kutaka serikali iwalipe.

"Kesi kama hii tumeipata leo asubuhi (jana) kutoka Kinyerezi mtu huyo amevunja nyumba yake na kusingizia mabomu,hiyo tumeiona na kuifanyia kazi," alisema Bw. Sadiki.

Mkazi huyo alitumia nyundo kuvunja nyumba yake ili ithaminiwe kuwa imetokana na mabomu ili serikali imlipe fidia lakini wakati akifanya hivyo majirani zake walimuona.

Bw. Sadiki aliwataka wananchi kuacha ujanja ujanja ambao utachelewesha kazi ya uthamini wa nyumba hizo ambayo itaanza Jumatatu.

Katika hatua nyingine, wahisani kutoka taasisi mbalimbali za umma na binafsi wanaendelea kumiminika kutoa misaada mbalimbali kwa waathirika wa mabomu ya Gongolamboto, Dar es Salaam.

Misaada hiyo ya vyakula, nguo, mahema na vifaa vya shule kwa ajili wa waathirika, vinapokewa na Bw. Sadiki ambaye hata hivyo alisema bado kunahitajika misaada mingi kwa sababu mahitaji ni mengi.

Kati ya taasisi zilizotoa misaada hiyo jana kwa Kamati ya Maafa ni Chama cha Wafanyakazi wa Elimu ya Juu (THTU) kilitoa daftari na kalamu zenye thamani ya sh. mil. 1.7 kwa ajili ya wanafunzi ambao vifaa vyao vimeungua.

Katibu Mkuu wa THTU, Bw. Kulu Maswanya alisema msaada huo umechangwa ili kuwarejesha wanafunzi walioathirika na mabomu katika hali ya kawaida kielimu.

Wengine walifika kutoa misaada ni Jumuiya ya Kiislamu ya Istiqaama Tanzania iliyokabidhi magodoro, unga wa sembe, nguo na ndoo vyote vikiwa na thamani ya sh. mil. 13.2.

Pia Benki ya wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam (DCB) ilitoa unga, mchele na maharage vyenye thamani ya sh. mil. 5 na kuahidi kuwa karibu na waathirika katika kipindi chote cha majonzi.

Mkurugenzi Mtendaji wa DCB, Bw. Edmund Mkwawa alisema benki hiyo ambayo inayo matawi matano imeona ni vyema iwasaidie wananchi wote waliopata janga hilo bila kujali kuwa ni mwanachama wa benki hiyo.

Waliochangia misaada ya mabomu ya Gongolamboto ni wanafunzi wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii waliochangia sabuni, unga, mchele na nguo vyenye thamani ya sh. 200,000.

Pia Kampuni ya Coast Millers Ltd iliyotoa unga wa sembe magunia 100 na unga wa ngano mifuko 50 na Kampuni ya Sandvick Mining Construction iliyotoa mahema 18 yenye thamani ya sh. mil. 6.5.

No comments:

Post a Comment