25 February 2011

Shahidi aeleza BOA ilivyoishtukia DECI

Na Rehema Mohamed

SHAHIDI wa kwanza katika kesi inayowakabili vigogo watano wa kampuni ya Development Entrepreneurship Community Initiative (DECI) Bw. Godriving Maro amesema
kuwa walienda kufanyia ukaguzi taasisi hiyo baada ya kugundua kuwa mchanganua wa biashara waliouwasilisha katika Benki ya Afrika (BOA) wakati wa kufungua akaunti hauendani na kiwango cha fedha walichokuwa wakiingiza benki.

Bw. Maro kwa sasa ni mfanyakazi wa Benki ya Standard Chater kwa sasa mwaka 2005 hadi Julai 2010 alikuwa akifanya kazi katika Benki ya Afrika (BOA) akiwa kama mkagunzi wa nyaraka za kufungulia akaunti zinazopelekwa na wateja wakati wa kufungua akaunti zao.

Bw. Maro aliyasema hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi Stuart Sanga, anayesikiliza shauri hilo.

Bw. Maro alisema hatua ya kufanya ukaguzi huo ilikuja  siku moja baada ya wakurugenzi wa DECI kuingiza dola 200,000 katika akaunti yao na kuwafanya waingie wasiwasi.

"Wakati wanakuja kufungua akaunti walisema wanajihusisha na biashara ya SACCOS, yaani kutoa mikopo lakini tulipowatembelea kupata ufafanuzi na chanzo chao cha fedha hawakutoa majibu ya kuridhisha," alisema Bw. Maro.

Alisema siku chache baadaye wakurugenzi wa DECI walikwenda BOA kuchukua zaidi ya sh. bilioni moja taslim, wakakataliwa.

Alisema kutokana na hatua hiyo, benki ilipelekewa barua kutoka kampuni wanasheria wa Azania Law Chamber ikiwataka watoe fedha hizo, pia wakakataliwa kupewa fedha taslimu bali wawasilishe akaunti nyingine ili fedha hizo ziweze kuhamishiwa.

Baada ya maelekezo hayo, Wakurugenzi wa DECI waliwasilisha akaunti ya Jisous Christ ya Dar es Salaam Community Bank na fedha hizo kuhamishiwa huko na kubakisha kiasi cha sh. milioni 167. Baadaye alisema akaunti hiyo iliwekwa katika orodha ya kufungwa wakisubiri maelezo kutoka serikalini.

Washitakiwa hao ni Jackson Mtares, Dominick Kigendi, Timotheo Ole Loitg’nye, Samwel Mtares na Mhasibu na Msemaji wa kampuni hiyo, Arbogast Kipilimba.

Vigogo hao wanakabiliwa na mashtaka ya kuendesha na kusimamia mradi wa upatu na kupokea amana kutoka kwa umma bila leseni.

No comments:

Post a Comment