Na Mussa Soraga, Zanzibar
HATIMAE Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA), kimepitisha rasmi azimio la kubadilisha mfumo wake wa Ligi Kuu ambayo sasa itaanza Agosti na
kumalizika Mei mwakani.
Kamati ya Utendaji ya chama hicho iliyokutana mjini hapa juzi kujadilii ombi hilo, imekubali kubadilisha mfumo wa zamani wa ligi hiyo baada ya kulikubali ombi la umoja wa klabu za soka kutaka mfumo huo ubadilike ili ligi hiyo ilete msisimko.
Hata hivyo ZFA imesema, utaratibu huo mpya kwa mwaka huu utatumika kwa timu 12 za Ligi Kuu ya Zanzibar, huku ligi za daraja nyingine yaliyosalia zitaendelea na utaratibu wa zamani wa kuanza michuano ya ligi kuanzia Januari hadi Agosti.
Akizungumza mjini hapa jana Katibu Msaidizi wa ZFA, Masoud Attai alisema kuwa pamoja na chama chake kuukubali mfumo huo mpya, kwanza itachezwa ligi ndogo ya mkondo mmoja kwa ajili ya kumpata bingwa mpya wa mwaka 2012.
Alisema ligi hiyo ndogo itaanza Mei na kumalizika mwishoni mwa Juni, ndipo baadaye itachezwa Ligi Kuu nyingine ya mikondo miwili Agosti kwa ajili ya kutafuta bingwa mwingine wa Zanzibar wa mwaka 2013.
Attai alisema, ZFA imefikia hatua hiyo baada ya kuzingatia kwamba hivi sasa timu zote zimekwishakamilisha taratibu zote muhimu za usajili ikiwa ni pamoja na kufanya uhamisho wa wachezaji, hiyvo isingekuwa vyema ligi ichezwe Agosti moja kwa moja kwa sababu zingekaa muda mrefu.
Alisema kwaba awali ombi hilo lilipowasilishwa katika ofisi yake, halikupata baraka za Kamati ya Utendaji kutokana na kuutilia mashaka mfumo huo kuwa ukikubalika utavuruga kalenda ya chama chake, ambayo inakwenda sambamba zile za Shirikisho la Mpira wa Miguu ya Afrika (CAF) na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
No comments:
Post a Comment