Na Zahoro Mlanzi
MABINGWA wa Ligi Kuu ya soka ya Zambia, ZESCO United inatarajia kujipima na wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa, Simba na Yanga katika michezo itakayopigwa Jumamosi na Jumapili Uwanja wa
Uhuru, Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mratibu wa michezo hiyo, George Wakuganda alisema timu hiyo itawasili nchini kesho na ndege ya Shirika la Ndege la nchini humo ikiwa na kikosi kamili.
Alisema wachezaji 20 pamoja na viongozi saba, ndiyo watakaounda kikosi hicho ambapo kwa sasa timu hiyo ndiyo mabingwa wapya katika ligi ya nchini humo.
"Mabingwa hao wa Zambia, watacheza na mabingwa wa Tanzania Bara, Simba siku ya Jumamosi na Jumapili watacheza na Yanga, katika michezo ambayo ninaamini itakuwa ni kipimo tosha kwa timu hizo katika maandalizi yao ya michuano ya kimataifa," alisema Wakuganda.
Mbali na mchezo huo, Wakuganda alisema Jumatatu Simba itashuka tena uwanjani kuumana na SOFAPAKA kutoka Kenya, ambayo inatarajia kutua nchini Ijumaa ikiwa na kikosi kamili.
Alisema michezo yote hiyo itakuwa na kiingilio kimoja ambapo Viti Maalum (VIP) sh. 15,000, Jukwaa Kuu sh. 10,000, Jukwaa la Kijani sh. 5,000 na mzunguko ni sh. 3,000.
ZESCO imetwaa ubingwa ikiwa na pointi 60 na michezo miwili mkononi ambapo timu inayofuata, Nchanga Rangers ina pointi 53 na kwa upande wa SOFAPAKA wao wamemaliza ligi wakiwa katika nafasi ya nne nyuma ya mabingwa Ulinzi.
No comments:
Post a Comment