KIGALI, Rwanda
TIMU ya taifa ya Gambia imepata kichapo cha nguvu katika michuano ya Afrika kwa vijana wenye miaka chini ya 17, baada ya kufungwa mabao 3-0 na Congo juzi.Ikiwa ni siku ya pili tangu kuanza kwa mashindano hayo nchini
Rwanda, mechi hiyo ilipigwa kwenye Uwanja mpya wa Umuganda mjini Gisenyi uliopo mpakani mwa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Gambia watatakiwa kushinda mechi dhidi ya Mali na Ivory Coast, ili iweze kusonga mbele kwenye michuano hiyo.
Congo ilipata bao la kwanza dakika ya saba kupitia kwa Samarange Binguila na bao la pili lilitumbukizwa kimiani dakika tatu baadaye na Stevy Epako.
Binguila alimalizia shangwe kwa kufunga bao la tatu dakika ya 51 na kuwamaliza nguvu wapinzani wao.
Uwanja huo mpya wenye uwezo wa kuingiza mashabiki waliokaa kwenye viti 6000, ulizidiwa na mashabiki, Ivory Coast ilitoka nyuma na kuichapa Mali mabao 2-1.
Ivory Coast walichapwa bao dakika ya 25, lililofungwa na Tiecoro Keita. Lakini walitulia na kufanya mashambulizi yaliyozaa bao la kusawazisha dakika ya 47, kupitia kwa Drissa Diarrassouba.Ushindi wa Ivory Coast, ulipatikana dakika ya 70, kwa njia ya penalti iliyopigwa na Stephane Bedi.
Kesho katika Kundi A, litakuwa na mechi kati ya wenyeji Rwanda na Misri, wakati Burkina Faso wataumana na Senegal, mshindi atajiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele, wakati atakayefungwa atakuwa katika nafasi ya kutoka.
Timu mbili katika kila kundi, zitakazofuzu kucheza nusu fainali, zitakata tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia kwa vijana wenye miaka chini ya 17 nchini Mexico, Juni mwaka huu.Hii ni mara ya pili katika miaka miwili, Rwanda kuandaa fainali za Afrika, mwaka juzi iliandaa fainali za vijana wenye miaka chini ya 20.
No comments:
Post a Comment