Na Suleiman Abeid, Shinyanga
MKAZI wa eneo la New Stand Manispaa ya Shinyanga aliyetambuliwa kwa jina la Bw. Haji Omari (30) amekufa papo hapo baada ya kuruka kutoka ndani ya gari la polisi wakati akijaribu kutoroka.Kwa mujibu wa mashuhuda wa
tukio hilo lililotokea juzi saa 1.10 usiku eneo la shule ya Sekondari ya Uhuru mjini Shinyanga, Bw. Omari aliruka kutoka ndani ya gari la polisi aina ya Toyota Land Cruiser namba PT. 1805 ambapo alianguka chini na kupasuka kichwa.
Mashuhuda walieleza kuwa marehemu alikamatwa na polisi baada ya kusababisha ajali mbili tofauti katika eneo la Kambarage Manispaa ya Shinyanga wakati akiendesha
gari aina ya Toyota Chaser yenye namba T. 901 ANL mali ya Bw. Omari Magoma.
Hata hivyo, ilidaiwa kuwa ajali hiyo ilitokana na yeye kuendesha gari akiwa amelewa hivyo alimgonga mfanyabiashara wa ndizi Bi. Doris Auko (60) mkazi wa Kambarage aliyekuwa amepanga ndizi zake kando ya barabara eneo la kanisa la A.I.C Kambarage.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Bw. Diwani Athumani alithibitisha kutokea kwa kifo hicho ambapo alisema ajali ya kwanza ilitokea eneo la Japanes corner ambapo Bw. Omari aliligonga gari aina ya Toyota Chaser kutokana na mwendo mkali aliokuwa nao na hata hivyo hakuweza kusimama.
“Sasa baada ya kuligonga gari hilo la kwanza ambalo hata hivyo polisi hawakuweza kupata namba wala jina la dereva wake, huyu bwana aliendelea kuendesha gari lake kwa
mwendo kasi lakini alipofika eneo la kanisa la A.I.C Kambarage aliligonga gari jingine lenye namba T. 192 AAB Toyota Chaser ambalo liliharibika vibaya lakini pia alimgonga muuza ndizi aliyekuwa jirani ambaye alizimia na kukimbizwa hospitali," alisema.
Alisema hata hivyo wakati gari hilo linaelekea katika kituo cha polisi dereva huyo akiwa amepakiwa nyuma pamoja na polisi watatu wawili wakiwa na silaha huku mmoja akimshikilia, ghafla alimsukuma polisi aliyekuwa na silaha na yeye akajirusha nje ambapo alianguka na kupasuka kichwa na kufa papo hapo.
Alisema polisi inaendelea na uchunguzi wa kina kuhusiana na tukio hilo na uchunguzi wa awali unaonesha chanzo chake ni dereva huyo kuendesha gari akiwa amelewa ambapo amewataka madereva wote kuheshimu sheria za
barabarani na kwamba wanapokuwa wamelewa wasiendeshe gari.
No comments:
Post a Comment