*Minziro kuongoza majeshi kesho
Na Elizabeth Mayemba
UONGOZI wa Yanga umesema licha ya Kocha wake Mkuu, Kostadin Papic kutangaza kubwaga manyanga kuifunza timu hiyo, wao
bado wanamtambua kama kocha wao kwa kuwa hajaandikia barua ya kuachia ngazi.
Papic wiki alitangaza kubwaga manyanga kuifunza timu hiyo kwa madai kwamba uongozi haumshirikishi katika mambo ya kiufundi ikiwemo kumwajiri Kocha Msaidizi, Felex Minziro.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Louis Sendeu alisema pamoja na kocha huyo kutangaza kujiuzulu, lakini uongozi wa Yanga haujapata taarifa yoyote ya maandishi.
"Kisayansi ni kwamba Papic, bado ni kocha wetu kwa kuwa hajawasilisha barua yoyote inayosema amejiondoa Yanga, muhimu ni yeye kuandika barua na kuleta kwa uongozi ili tuweze kuipitia kisheria," alisema Sendeu.
Alisema ni kweli suala la yeye kujiuzulu si geni kwa kuwa amekuwa akitangaza mwenyewe kwenye vyombo vya habari na isitoshe alikwenda kuwaanga na wachezaji wake, lakini pamoja na yote hayo hajawasilisha barua.
Yanga ipo kambini kujiandaa na mchezo wake wa kesho wa michuano ya CAF dhidi ya Dedebit ya Ethiopia, lakini ikiwa na Minziro ambaye atakuwa na jukumu ya kuliongoza jeshi hilo la Jangwani akiwa na Meneja wake Salvatory Edward.
Katika hatua nyingine, Dedebit ambayo jana ilifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam wametamba kuibuka na ushindi katika mechi hiyo.
No comments:
Post a Comment