*'Mashushu' wao watua Dar
Na Zahoro Mlanzi
WAPINZANI wa timu ya Yanga katika michuano ya Kombe la Shirikisho, Dedebit FC kutoka Ethiopia, imepata pigo baada
ya kipa wao wa kutumainiwa Jemal Tassew kuwa nje ya uwanja kwa mwezi mmoja.
Kipa huyo ambaye pia ndiye kipa namba moja wa timu ya Taifa ya Ethiopia, ameumia mguu wa kulia na mkono wa kushoto, hivyo kuikosa Yanga, kwani atalazimika kuuguza majeraha kwa muda huo.
Mbali na kipa, kiungo Fitsum Teferi atakuwa nje ya uwanja kwa muda usiojulikana baada ya kupata maumivu ya bega wakati wa mazoezi.Kwa mujibu wa taarifa za mtandao wa klabu hiyo, zilieleza kwamba kipa Tassew kwa sasa amefungwa bendeji gumu (POP) na anatibiwa katika hospitali ya Yordanos iliyopo katika jiji la Adis Ababa nchini humo.
"Imebainika kwamba mguu pamoja na mkono wake utafungwa bendeji gumu (POP) na hatafanya tena mazoezi kwa mwezi mmoja mpaka bendeji hizo zitakapotolewa," alieleza daktari wa timu hiyo kupitia mtandao wao.
Daktari huyo alieleza kwamba pia kiungo Teferi atakuwa nje ya uwanja kwa muda usiojulikana kutokana na kuumia bega wakati wa mazoezi na kwamba hali yake si nzuri.
Katika hatua nyingine, Ujumbe wa watu watatu ukiongozwa na Kocha Msaidizi Endrius Birhanu umetua jijini juzi usiku kuipeleleza Yanga.Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam (JNIA), uliwashuhudia watu hao wakiomba msaada kwa madereva wa taksi waliopo uwanjani hapo kuchaguliwa hoteli nzuri huku wakiwa na kiu ya kuijua Yanga.
"Tumetoka Ethiopia na tupo hapa kwa wiki moja na baadaye tutarudi nchini kwetu, tunaomba mtusaidie kupata hoteli nzuri na vipi kuhusu timu yenu ya Yanga ni nzuri sana, tunataka kuiona jinsi itakavyocheza na timu yetu," kilisema chanzo.
No comments:
Post a Comment