19 January 2011

Wapeni wananchi taarifa za maendeleo- RC Babu

Na Livinus Feruzi, Bukoba
 
MKUU wa Mkoa wa Kagera Bw. Mohamed Babu amewataka wenyeviti na watendaji wa vijiji mkoani Kagera kuitisha na kufanya vikao na mikutano ya mara kwa mara ili kuwafahamisha wananchi mambo mbalimbali ya
maendeleo yanayofanywa na serikali yao.
 
Bw. Babu alitoa agizo hilo juzi ofisini kwake wakati akizungumza na watendaji wa Kampuni ya Business Times Ltd inayomiliki magazeti ya  Majira, Business Times, Dar Leo na Spoti Starehe  waliko ziarani mkoani Kagera kwa lengo la kuhamasisha wadau mbalimbali katika maendeleo.

Alisema kuwa kuna tatizo la wananchi kutopata habari zinazohusu maendeleo yao na kuwa tatizo hilo linatokana na baadhi ya watendaji wa vijiji kutoitisha mikutano, ambapo taarifa mbalimbali za maendeleo zinatolewa  na viongozi katika ngazi za mkoa, wilaya na kata na kuongeza kuwa tatizo hilo linakuwepo kutoka kwenye kata kwenda kwa wananchi.
 
“Tatizo la wananchi kukosa habari za maendeleo ni kubwa kutoka kwenye kata kwenda kwa wananchi na hii inatokana na sehemu mbalimbali kutofanya vikao na mikutano,” alisema Bw. Babu
 
Bw. Babu alisema wenyeviti wakifanya mikutano ya mara kwa mara itasaidia wananchi  kupata habari zinazohusu maendeleo.
 
Alisema licha ya kwamba wilaya mbalimbali za mkoa wa Kagera zina redio lakini bado mambo mengi hayafahamiki kwa wananchi na kuwa yanahitajika magazeti ambayo yatasaidia kuongeza msukumo wa upatikanaji wa habari kwa wananchi wote mkoani hapa.
 
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa habari za Kanda ya Magharibi zinazochapishwa na gazeti la Majira zitasaidia kuchochea maendeleo mikoa ya kanda hiyo ukiwemo Kagera.
 

No comments:

Post a Comment