LONDON, England
WAKALA wa mchezaji Andrey Arshavin, Dennis Lachter amezikana tetesi zinazomuhusisha nyota huyo wa Arsenal, kutimkia katika Klabu ya Juventus ya Italia.Mchezaji huyo wa kimataifa raia wa Russia, amebakiza miaka miwili
na nusu katika Klabu hiyo ya Gunners, baada ya kuwasili katika klabu hiyo inayotumia Uwanja wa Emirates mwaka 2009, lakini kwa sasa amekuwa akiripotiwa kutaka kukimbilia kwa vinara hao wa ligi ya Serie A.
Lakini hata hivyo wakala wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29, Lachter alisema jana hakuna makubaliano yaliyofikiwa na akasisitiza kuwa Arshavin, anajisikia mwenye furaha Arsenal katika harakati za timu hiyo kuwania taji la Ligi Kuu.
"Kuna uwezekano wa Arshavin kuhamia Juventus," Lachter aliiambia tovuti ya michezo ya Russia. "Lakini kuna mambo mawili ya kuzuia mkataba huo," aliongeza.
"Kwanza Arsenal mwaka huu inaweza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu. Medani hiyo ya dhahabu kwenye ligi ya Uingereza ndiyo ndoto ya kila mchezaji.
"Pili uwezo wa kifedha wa Juve na kiasi ambacho Arsenal, inakitaka ili kumwachia Arshavin si chini ya dola milioni 26 sawa na pauni milioni 17," aliongeza na akasema kuwa kwake yeye ni vigumu kuzungumza chochote kwa sababu mchezaji huyo bado ana mkataba wa miaka miwili na nusu na Arsenal na hakuna ofa ya kueleweka.
Alisema kwa mawazo yake anadhani ni uvumi tu na akasema kuwa Juventus ingekuwa imeshamchukua Arshavin miaka miwili na nusu iliyopita, lakini hawakuweza kufanya hivyo.
No comments:
Post a Comment