03 January 2011

Wachezaji Toto washindwa kuingia kambini

Na Addolph Bruno

KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Toto African ya Mwanza, Choki Abeid, ameshitushwa na kitendo cha baadhi ya wachezaji wake kushindwa kuripoti kambini kujiandaa na Ligi Kuu Bara hatua ya lala salama.Timu hiyo ilianza kambi baada ya
sikukuu ya Krismasi, ikiwa na wachezaji tisa waliorejea kutoka kwao, kwa ajili ya kujiandaa na mzunguko wa pili.

Akizungumza na Majira kwa simu jana, akiwa jijini Mwanza, kocha huyo alisema wachezaji walioripoti kambini ni tisa, na wengi wao wakiwa bado hawajawasili na hawajatoa taarifa yoyote.

"Mpaka sasa wachezaji wetu wengi kutoka mikoani hawajawasili, walioripoti ni  wa hapa Mwanza, hatuna taarifa zao,¡± alisema.

Alisema aliamua kuliweka wazi suala hilo kwani timu inapofanya vibaya, kocha huwa wa kwanza kulaumiwa.

Alisema wachezaji ambao hawajaripoti ni kutoka Dar es Salaam na Shinyanga, wanawasubiri ili waanze programu nzima ya mazoezi.
Kocha huyo alisema wataendelea kuwasubiri mpaka timu yao ya vijana wenye miaka chini ya 20, itakaporejea jijini Mwanza ikitokea Dar es Salaam, kwenye michuano ya Kombe la Uhai.

Choki aliongeza kuwa, programu aliyoiandaa haitafaa huku akiwa na hofu wa kutofanya vizuri kwa kikosi chake katika mzunguko wa lala salama.
Alisema aliandaa programu iliyoonesha watakuwa na mechi tatu za kirafiki kujiandaa na mzunguko wa pili, lakini michezo hiyo kuna uwezekano wa kutochezwa.

No comments:

Post a Comment