05 January 2011

Vigogo 4,700 hawajataja mali zao

Rabia Bakari na Rose Itono

ZAIDI ya viongozi wa kisiasa na wa umma 4,700 hawajeresha fomu zinazotaja mali zao kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, ghivyo kuwa katika hatihati ya
kuchukuliwa hatua za kisheria.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini jana, Kamishna Mkuu wa Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Salome Kaganda alisema jumla ya viongozi wa siasa waliotumiwa fomu hizo ni 4,346 ambao kati ya hao ni 1,446 ndio waliorejesha huku 3,047 bado wakiwa hajawarejesha fomu hizo.

Aidha kwa upande wa viongozi wa umma, waliotumiwa fomu hizo ni 4,064 ambao kati ya hao 2,324 wamerejesha na 1,741 wakiwa bado wanadaiwa fomu hizo.

Alisema idadi kubwa ni ya wanasiasa ambao hawajarejesha fomu inasababishwa na madiwani ambao taratibu za uteuzi na uundwaji wa mabaraza ya halmashauri kutokamilika.

"Hadi kufikia Desemba 31, mwaka jana, jumla ya madiwani 2,844 sawa na asilimia 73.37 hawarejesha fomu.

Taratibu za kuwafikia zinaendelea kufanyika ili kila muhusika aweze kuwajibika kutekeleza sheria," aliongeza.

Ukiondoa madiwani, viongozi waandamizi wa siasa 56 sawa na asilimia 11.9 hawakurejesha fomu kwa wakati.

Jaji Kaganda alisema kwa upande wa viongozi wa umma, idadi kubwa ya mahakimu wa mahakama za mwanzo na wilaya ambao wanakadiriwa kufikia 1,631 sawa na asilimia 40.13 hawakurejesha fomu kwa wakati kutoka na hali ya kijiografia na ugumu wa mawasiliano.

Kwa mujibu wa sheria za maadili ya viongozi wa umma, namba 13 ya mwaka 1995, inawataka viongozi kuwasili silisha tamko lao ndani ya siku 30 baada ya uteuzi, kila mwisho wa mwaka na baada ya kuacha wadhifa.

"Sheria inamtaka kiongozi yeyote wa umma kutoa tamko rasmi kuhusu mali na madeni yake, mke au mume na watoto walio chini ya miaka 18 ambao hawajaoa wala kuolewa," alifafanua Jaji Kaganda.

Akitaja hatua zitakazochukuliwa kwa wale wasiowasilisha fomu hizo kwa wakati, Jaji Kaganda alisema Sekretarieti ya maadili itawahoji wahusika kwanini wasichukuliwe hatua zaidi kwa mujibu wa sheria, na kama maelezo hayatoridhisha, viongozi husika wataitwa mbele ya Baraza la Maadili ambalo litawasikiliza na kutoa mapendekezo kwa kamishna wa maadili juu ya hatua zinazofaa kuchukuliwa.

"Taarifa ya baraza itawasilishwa kwa mheshimiwa rais na nakala kwa Spika wa bunge kwa hatua mbalimba za kiutumishi na kiutawala, pia tutasimamia kwa nguvu utekelezaji wa sheria kwa viongozi kuhakikisha kuwa Mamlaka za Nidhamu za Viongozi husika zinawajibika ipasavyo kutekeleza mapendekezo ya Sekretarieti dhidi ya viongozi wasiotekeleza misingi ya maadili,"alisema.

Aliongeza kuwa, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi imejidhatiti kutoa elimu ya mara kwa mara kwa viongozi wa Umma  ili kuongeza mwitikio wa urejeshaji wa fomu za Tamko.

"Viongozi wa Umma wanahitaji kupewa elimu mara kwa mara kuhusu sheria ya Maadili ya uongozi ili wafahamu wajibu wao wa kuzingatia kanuni za maadili",alisema Jaji Kaganda.

Aliongeza kusisitiza kuwa, mkazo utatiliwa katika kutoa elimu ya maadili kwa viongozi waliochaguliwa au kuteuliwa kufuatia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2010.

No comments:

Post a Comment