13 January 2011

Uwanja wa ndege Mwanza kukarabatiwa

Na Wilhelm Mulinda, Mwanza

SERIKALI inaandaa mpango wa kuongeza urefu wa uwanja wa ndege wa Mwanza kwa ajili ya kuwezesha ndege kubwa za mizigo kutua ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo kutoka jiji hilo kwenda nje ya nchi.Kauli hiyo ilitolewa jana na
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Bw. Lazaro Nyalandu wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza wakati alipokuwa ziarani mkoani humo.

Bw. Nyalandu alisema kuwa kwa sasa kutokana na uwanja huo kuwa mdogo, viwanda vinavyosindika minofu ya samaki jijini Mwanza vinalazimika kusafirisha bidhaa hiyo nje ya nchi kupitia uwanja wa ndege wa Nairobi nchini Kenya ambako ndege kubwa za mizigo kutoka nchi mbalimbali zinatua.

Pia alisema kuwa hatua hiyo itawezesha jiji hilo kuwa na usafiri wa uhakika wa anga kwa ajili ya kuhudumia nchi za Maziwa Makuu.

Katika hatua nyingine, waziri huyo alisema kuwa serikali inaandaa mpango wa kuratibu wafanyabiashara ndondogo maarufu kama wamachinga na kuhakikisha kwamba wanafanya shughuli zao katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili hiyo kwa faida yao wenyewe pamoja na taifa kwa ujumla.

Alisema kuwa kitendo cha kuacha wamachinga kuendesha shughuli zao bila utaratibu maalumu kinasababisha mapato ya serikali kuvuja kwa vile wakati mwingine wafanyabiashara hao wanauza vitu vipya vyenye mitaji mikubwa vinavyotolewa madukani na kwamba baada ya kuuza fedha hizo huwasilishwa katika maduka hayo bila kulipia kodi.

"Unakuta mtu anapanga mabegi mengi barabara tena mapya au duka zima la vitabu linapangwa barabarani na biasahara inafanyika bila kulipa kodi eti kwa kisingizio cha umachinga kumbe mali hiyo imetoka madukani.

Kwa kweli kufanya hivyo ni kuipotezea serikali mapato hivyo, ni lazima uwepo utaratibu wa kuwatambua wamachinga, maeneo waliopo pamoja na aina ya biashara wanayofanya ili kudhibiti kodi," alisema.

Pia akitoa mafano, waziri huyo alisema kuwa kuna biashara kubwa inayofanyika katika Soko la Samaki la Kimataifa la jijini Mwanza ambapo unakuta mtu ana begi lililojaa pesa kwa ajili ya kununulia samaki, lakini serikali haifaidiki na biashara hiyo kwa kisingizio cha umachinga.

No comments:

Post a Comment