Na Eliasa Ally, Iringa
WANACHAMA wa Sao Hill Forest Industry Association (SAFIA) iliyopo katika Wilaya ya Mufindi wamesema kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Bw. Ezekiel Maige amedanganywa na viongozi wa chama hicho alipofika kusikiliza matatizo
yao.
Waziri Maige alifika Sao Hill kusikiliza mgogoro huo lakini wanachama wanadai mkutano huo ulishirikisha watu wachache badala ya wote wanaohusika katika uvunaji wa magogo ili aweze kubaini ukweli halisi.
Wananchama hao wamemtaka Waziri Maige afanye ziara nyingine ili akutane na wanachama wote 580, viongozi wa SAFIA na utawala wa Sao Hill ili kumaliza mgogoro uliopo kwa sasa na kuwezesha wanachama kupata faida wanayoitarajia.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana mjini Mafinga wanachama waliutupia lawama uongozi wa SAFIA kufanya mambo bila kuwashirikisha, kwa masilahi yao binafsi na kutumia nguvu kudidimiza wenzao.
"Uongozi huu wa SAFIA sasa unatugonganisha na utawala wa Sao Hill, wanachama na Waziri Maige. Tatizo lililopo ni uongozi wenyewe wala siyo wanachama, wala siyo utawala wa Sao Hill, hao wana ajenga zao binafsi," walisema.
Wakizungumza huku wakitaka majina yao kuhifadhiwa, walisema kuwa viongozi hao walifanya kikao na Waziri Maige Januari 6, 2011 bila kuwashirikishwa, hivyo kuwanyima haki yao ya kutoa dukuduku zao.
Walisema kuwa kimsingi Waziri Ezekiel Maige alipotoshwa kwa taarifa kuhusu mgogoro aliyopatiwa, na wamemwomba waziri huyo akutane na wanachama wote 580 ili asikie wazi maoni yao.Wanachama hao waliutupia lawama uongozi wa SAFIA na kuwataka wahusika wajiuzuru kutokana na kushindwa kufanya kazi za kikundi hicho kwa mujibu wa katiba yao.
Mwenyekiti wa SAFIA, Bw. William Nyalusi alipohojiwa kutofanya vikao halali alikiri kuwa tangu uongozi huo uingie madarakani haujawahi kuitisha mkutano wa wanachama wake wala kuwasomea mapato na matumizi.
Bw. Nyalusi pia alisema kuwa anatarajia kuitisha mkutano wa wanachama wa uvunaji magogo wa SAFIA mwishoni mwa mwezi huu na kuwa ziara ya Waziri Maige ilikuwa ya ghafla na alitaka kukutana na viongozi wa SAFIA na Sao Hill na si wanachama wote.
No comments:
Post a Comment